Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara
Taratibu zinazotumika kumpandisha cheo mtumishi wa umma zimeainishwa katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 kama ifuatavyo:-
i) Kuwepo kwa nafasi iliyotengewa fedha katika mwaka wa fedha husika,
ii) Muundo wa utumishi (scheme of service) wa kada husika,
iii) Utendaji mzuri wa kazi,
iv) Orodha ya ukubwa kazini (seniority list),
v) Maendeleo ya kitaaluma (career development),
vi) Urithishanaji wa madaraka (succession plan).
Vigezo vilivyotumika kupanga mishahara ya sasa ni ripoti ya zoezi la tathmini ya kazi (Jo Evaluation exercise) lililofanyika mwaka 1998.
Mtumishi wa umma anatakiwa awe na nakala ya vitu vifuatavyo ili aweze kulipwa pensheni;-
i.Barua ya kustaafu.
ii.Barua ya kuajiriwa kwa mara ya kwanza Serikalini.
iii.Barua ya kuajiriwa katika masharti ya kudumu na pensheni
iv.Barua ya kuthibitishwa kazini.
v.Barua ya kupandishwa vyeo mbalimbali wakati wote wa Utumishi Serikalini.
vi.Fomu ya ‘retiring award’.
Mtumishi wa umma anapaswa kuwa na vitu vifuatavyo katika kushughulikia masuala ya mirathi:-
i.Cheti halisi (original) cha kifo kilichotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo.
ii.Hati halisi (original) ya msimamizi wa mirathi iliyobandikwa picha ya msimamizi.
iii.Nakala ya cheti cha ndoa.
iv.Kiapo cha mjane kinachotolewa na Mahakama na chenye picha ya mjane.
v.Kiapo cha kutunza watoto chenye picha ya anayetunza watoto kinachotolewa na Mahakama.
vi.Nakala ya Vyeti vya kuzaliwa watoto wa marehemu wenye umri usiozidi miaka 21.
vii.Picha mbili (passport size) za msimamizi wa mirathi,watoto wa marehemu na mjane zilizogongwa muhuri wa Mahakama.
Je, taratibu zipi zinazotumika katika kushughulikia makosa ya kinidhamu yanayoshughulikiwa kwa utaratibu rasmi (formal proccedings)?
Makosa yanayoshughulikiwa kwa utaratibu ulio rasmi (formal proccedings) yana hatua zifuatazo:-
(i)Mamlaka ya nidhamu inapaswa kufanya uchunguzi wa awali ili kujiridhisha kama iko haja ya kuchukua hatua za kinidhamu kabla ya kuanza mchakato wowote wa kinidhamu (Kanuni 36, Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003)
(ii)Iwapo mamlaka ya nidhamu itajiridhisha kuwa kosa limefanyika, basi itampa mtumishi Hati ya Mashtaka na Notisi kumweleza kosa/makosa anayotuhumiwa kufanya na anayolazimika kuyajibu kupitia utetezi wake(Kanuni 44(1), Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003)
(iii)Mamlaka ya nidhamu inaweza kumsimamisha kazi mtumishi ambaye suala lake la kinidhamu linashughulikiwa ili kuwezesha ushughulikiwaji wa suala hilo kufanyika (Kanuni 38 na 39 za Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003)
(iv)Ikiwa utetezi au majibu ya mtumishi anayetuhumiwa hautoshelezi kumtoa hatiani, mamlaka ya nidhamu itaunda Kamati ya Uchunguzi (Kanuni 45(1) Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003) kwa ajili ya kuchunguza suala hilo ikiwa ni pamoja na kumhoji mtumishi husika, mashahidi n.k.
(iv)Kama majibu ya mtumishi baada ya kupokea Hati ya Mashtaka yanaonyesha kukubali kutenda kosa, mamlaka ya nidhamu haitalazimika kuunda Kamati ya Uchunguzi na itaendelea kutoa adhabu stahiki (Kanuni 45(3) Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003).
Kwa mujibu wa Kanuni K.17 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, Mtumishi wa Umma aliyepewa Rufaa ili kumwezesha kutibiwa Nje ya kituo chake cha kazi anastahili kulipwa Posho ya Kujikimu.
Kwa mujibu wa Maelekezo ya Katibu Mkuu (Utumishi) katika barua yenye Kumb.Na.CAC.45/257/01/A/83 ya tarehe 9/9/2013 mtumishi anastahili kupandishwa cheo baada ya kutumikia cheo cha awali kwa kipindi cha angalau miaka mitatu (3) kwa kuzingatia TANGE (Seniority list) iliyopo, Sifa za Kimuundo, Kuwepo kwa nafasi iliyoidhinishwa katika Ikama na kuwepo kwa fedha za kugharamia upandishwaji vyeo kwenye bajeti.
Kwa mujibu wa Kanuni J.2, L.5 na L.13 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 mtumishi anayehamishwa anastahili ya kulipwa posho ya kujikimu kwa siku kumi na nne (14) kwa ajili yake, mwenzi, na hadi watoto wanne; Posho ya usumbufu na Mizigo yake tani tatu (3). Hata hivyo Kwa mujibu wa Kanuni L.8 ya kanuni hizo kwa watumishi wanaojiombea uhamisho mwajiri ana hiari ya kumlipa au kutomlipa kutokana na mazingira ya uhamisho wake pamoja na upatikanaji wa fedha.
Kwa mujibu wa Kanuni H.5 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009; Nauli ya Likizo hulipwa mara moja katika mzunguko wa miaka miwili. Nauli hiyo hulipwa kwa mtumishi, mwenzi na wategemezi wasiozidi wanne kwa kuzingatia viwango vya nauli vinavyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Walimu walioajiriwa kwa Mkataba (Leseni), wanatakiwa kujiendeleza katika fani ya Ualimu (Elimu) ndani ya kipindi cha miaka mitano kuanzia 2007 hadi 2012. Hivyo kama amejiendelea katika fani ambayo siyo ya Ualimu anatakiwa kutafuta ajira upya Serikalini kwa kutumia fani aliyosomea na sio kubadilishwa kazi.