Habari
WITO WATOLEWA WATUMISHI WA UMMA KUENDELEA KUJENGEWA UWEZO KIUTENDAJI ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA UMMA
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi ameielekeza Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ya Ofisi hiyo kuendeleza programu ya mafunzo kwa Watumishi wa Umma kila Jumatatu ya wiki kupitia wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Ofisi hiyo ili kuwajengea uwezo watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao utakaosababisha Ufanisi katika utoaji wa huduma na kuleta tija kwa jamii.
Bw. Daudi ameyasema hayo Machi 16, 2026 wakati akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora alipokuwa akihitimisha programu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi hao jijini Dodoma.
“Nipende kuwapongeza watumishi wenzetu walioendesha mada mbalimbali katika programu hii ya mafunzo kwa weledi, ujasiri, na umahiri mkubwa ili kuhakikisha uelewa unajengeka kwa watumishi wa umma na kuimarisha utendaji kazi kwa maslahi ya Taifa”. Bw. Daudi alisema
Aidha, amewasisitiza watumishi wa Ofisi yake kuutumia utaalamu walionao na uwezo wanaojengewa mara kwa mara kutekeleza majukumu yao kwa juhudi na ufanisi ili kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, SACP. Ibrahimu Mahumi amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI imeanzisha utaratibu wa kushirikishana uzoefu wa kitaalamu kwa watumishi wengine kwa kila Idara kupitia programu ya mafunzo ya kila wiki ili kujenga uelewa mpana utakaosababisha umahiri katika utendaji kazi.
Akiwasilisha mada inayohusiana na masuala ya Uhamisho katika Utumishi wa Umma, Afisa Utumishi Mwandamizi, kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Said Ally amesema lengo la kushirikishana uzoefu kwa wataalamu wa ndani ni kuhakikisha kila mtumishi ndani ya Ofisi hiyo anakuwa na uelewa utakaomuwezesha kuyajua majukumu ya kila Idara ili kutoa huduma kwa wananchi kwa uharaka na ubora zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Sera za TEHAMA na Viwango, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Ibrahim Toure, akiwasilisha mada ya Usalama Mtandaoni, amesema lengo la mada hiyo ni kukumbushana juu ya matumizi sahihi ya mifumo ili kuwa na mtazamo na utamaduni wa usalama mtandaoni wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na hata wawapo nje ya Ofisi.
Vilevile Afisa TEHAMA Mkuu, Idara ya TEHAMA Serikalini, Bi. Zalika Hussein amesema elimu ya usalama mtandaoni itawawezesha watumishi kuhakikisha mifumo na miundombinu ya TEHAMA na taarifa zinazohifadhiwa kwenye mifumo hiyo zinakuwa salama bila kufikiwa na watu wasiohusika kwa kuhakikisha wanatumia nywila zao wenyewe bila kumshirikisha mtu mwingine yeyote kwa lengo la kulinda taarifa za serikali ikiwa ni utaratibu wa kuhakikisha usalama, usiri, na uadilifu wa data za umma dhidi ya ufikiaji usioidhinishwa.
