Habari
WITO WATOLEWA KWA WATUMISHI WA UMMA KUBADILIKA KIMTAZAMO KATIKA UTENDAJI ILI KUFIKIA MALENGO YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi ametoa wito kwa Watumishi wa Umma nchini kubadilika kimtazamo katika utendaji ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwemo matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Bw. Daudi ametoa wito huo leo tarehe 13/10/2025 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo eneo maalum linalotumika kutoa mafunzo katika Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma, yanayofanyika kila siku ya Jumatatu kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao ili kuboresha Utendaji kazi.
Kaimu Katibu Mkuu Bw. Daudi amesema, Watumishi wa Umma kubadilika kimtazamo katika utendaji ni jambo muhimu kwani kunakuwa na ufanisi wa wa kazi unaowezesha kuwa na Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.
“Ninatoa wito kwenu, msitekeleze majukumu yenu kwa mazoea, kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mbadilike kiutendaji ili kuendana na mabadiliko yakiwemo ya kidijiti kwa kuleta ubunifu na mawazo chanya yatakayoiwezesha serikali kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA,” Bw. Daudi alisema.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano Serikalini kutoka Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Bw. Titus Kaguo wakati akiwasilisha mada kwa watumishi hao kuhusu Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika Taifa letu ambapo Dira hii imelenga kuwa kufikia mwaka 2050, asilimia 70 ya Watanzania watakuwa wanatumia mifumo ya TEHAMA na asilimia 80 ya huduma mbalimbali za kiserikali zitakuwa zikitolewa kidiji ili kuleta Ufanisi katika Utendaji.”