Habari
WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NI JUKWAA LA KUWAFIKISHIA WANANCHI HUDUMA ZA SERIKALI- Waziri Kikwete
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amesema Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu linalowawezesha wananchi kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali pamoja na namna ya kuzipata kwa urahisi.
Mh. Ridhiwani ameyasema hayo Juni 17, 2026 wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Utumishi ya Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema, maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa Taasisi za umma kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuonesha mafanikio, ubunifu na maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa huduma kwa umma.
Mhe. Ridhiwani amesema Serikali imeendelea kuimarisha Utumishi wa Umma kupitia maandalizi ya Programu ya Maboresho ya Utumishi wa Umma yenye lengo la kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa programu hiyo itajikita katika maeneo matano ya kimkakati ambayo ni mabadiliko ya fikra katika Sekta ya umma, ujumuishaji na ushirikishwaji wa Wananchi, uongozi na uwajibikaji, usimamizi wa Rasilimaliwatu pamoja na mageuzi ya huduma za kidijiti.
Vilevile Waziri Kikwete amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidijiti ikiwemo e-Utendaji, e-Watumishi, e-Mrejesho, e-Ardhi, e-Office, TAUSI, GePG, MUVU na MAJIIS ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali.
Akizungumzia Ustawi wa Watumishi wa umma, Mhe. Ridhiwani amesema Serikali imepandisha vyeo watumishi 219,000 waliokidhi vigezo katika mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao na kuongeza motisha kazini. Amesisitiza kuwa zoezi hilo liendelee kutekelezwa kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo ya Utumishi wa Umma ili kuhakikisha haki, usawa na uwazi vinazingatiwa kwa watumishi wote.
Katika eneo la ajira, Mhe. Kikwete amesema Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeajiri watumishi 42,500 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025/26. Aidha, amesema Serikali imetenga nafasi mpya 45,000 za ajira kwa mwaka wa fedha 2026/27 ili kuongeza nguvu kazi katika sekta mbalimbali za utoaji huduma.
Mhe. Kikwete amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na Ustawi wa Watumishi wa Umma kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba kwa watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu. Amesema Serikali tayari imekamilisha nyumba 54 kwa watumishi wa sekta za afya na elimu katika mikoa mbalimbali na inaendelea na ujenzi wa nyumba nyingine 78.
Kwa upande wake Katibu Mkuu-UTUMISHI Bw. Juma Mkomi amesema ushiriki wa Taasisi nyingi katika maonesho hayo unaashiria wingi wa Huduma zinazoendelea kutolewa na kuwasihi Wananchi kutembelea mabanda ya maonesho ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupata ufafanuzi wa masuala ya Kiutumishi na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA pamoja na huduma zingine kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI kama gazeti la Serikali.
