Habari
WHI IMELETA MAPINDUZI MAKUBWA KWA WATUMISHI WA UMMA KUMILIKI NYUMBA -Mhe. Simbachawene
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Watumishi Housing Investments (WHI) ni taasisi ambayo imefanya mambo makubwa kwani tangu kuanzishwa kwake limeleta mapinduzi makubwa kwa Watumishi wa Umma kuweza kumiliki nyumba bora kwa masharti nafuu, hatua inayolenga kuboresha hali ya maisha na kuongeza ufanisi kazini.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo katika eneo la nyumba zilizojengwa na WHI Njedengwa jijini Dodoma wakati akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma.
Mhe. Simbachawene amesema WHI imefanikiwa kutekeleza makazi kwa Watumishi wa Umma jumla ya nyumba 1006 katika mikoa 19 nchini lengo likiwa ni kutatua changamoto ya makazi inayowakabili Watumishi hao hususan wa kipato cha chini.
Amesema mpango huo ulibuniwa ili kuwapa nafuu watumishi kumiliki nyumba hizo ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha nyuma haikuwa rahisi kwa watumishi hao kumiliki nyumba kutokana na makampuni mengi yanayojihusisha na ujenzi wa nyumba kujiendesha kibiashara kwa lengo la kupata faida.
Amesema, shabaha kubwa ya WHI ni kujenga nyumba vijijini kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wa kipato cha chini wakiwemo Walimu na Wauguzi kuweza kumiliki nyumba pamoja na kujenga maeneo ya mijini ili kuwasaidia watumishi wenye kipato cha chini na ajira mpya kuacha kupanga nyumba mbali na maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Mhe. Augustine Holle amesema WHI ni Taasisi ambayo imekuwa ikijenga nyumba zinazouzika tofauti na Taasisi zingine kutokana na kujenga nyumba hizo kulingana na kipato cha wateja wake ambao ni Watumishi wa Umma
"WHI ni Taasisi makini ambayo imejikita kurahisisha umiliki wa nyumba kwa Watumishi wa Umma kuwa urahisi na endelevu " amesisitiza Mhe. Holle.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Dkt. Fred Msemwa amesema suala la makazi kwa Watumishi wa Umma ni jambo lisiloepukika kwani linachochea ufanisi wa kazi kwa Watumishi hao.
Amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kujenga nyumba za Watumishi kwa bei rahisi ili kuwawezesha Watumishi hao kuweza kumiliki nyumba hizo kwa kuzinunua kwa bei rahisi.
"Kwa mara ya kwanza haikuwa rahisi, nyumba zilizojengwa licha ya kuwalenga Watumishi lakini walikuwa hawawezi kuzinunua kutokana gharama yake kuwa juu ila kwa sasa Watumishi wamekuwa wakizifurahia," amesisitiza Dkt. Msemwa.
Utekelezaji wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ni dhamira pana ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya kumiliki makazi bora.