Habari
WAZIRI SIMBAWENE; MFUMO WA KIELEKTRONI NI USHINDI KATIKA KUTENDA HAKI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene amesema kitendo cha Serikali kuanza kutumia mfumo wa kielektroni wa Kukusanya, Kuchakata na Kutunza Kumbukumbu za Kesi Jinai (CMIS) ni ushindi katika utendaji haki kwa umma.
Mhe. George Simbachawene amesema hayo leo Jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa mfumo huo uliosanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
"Mfumo huo umekamilika katika wakati sahihi ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea na jitihada za kuimarisha utoaji haki kwa wananchi" ameongeza.
Vile vile, amebainisha kuwa mfumo huu umeunganishwa na mfumo unaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa (GovESB).
Amesema mifumo ya Taasisi za Haki Jinai kama vile Polisi, TAKUKURU na Mahakama imeunganishwa na inabadilishana taarifa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu mifumo ya Serikali kubadilishana taarifa.
Aidha, Mhe. Simbachawene ametumia fursa hiyo kuzihimiza Taasisi zote za Umma kutekeleza jitihada za serikali mtandao kwa kasi ili kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.
Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Pauline Gekul, amesema Wizara ya Katiba na Sheria imejizatiti kutekeleza jitihada za Serikali mtandao kwa kutengeneza mifumo madhubuti ya TEHAMA ili kutoa huduma bora kwa umma.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amesema kuzinduliwa kwa mfumo huo ni hatua kubwa katika kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi kwani jambo hilo halikuwa rahisi kufanyika kwa siku za nyuma.
‘’Mfumo huu unafungua ukurasa mpya katika kuelekea uchumi wa kidijitali huku tukifanikisha azma ya. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo yote ya utoaji haki inawasiliana ‘’ amesema Bw. Daudi.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylvester Mwakitalu, amesema mfumo huo utatunza kumbukumbu zote ikiwamo hati za mashtaka na hukumu na utakuwa na uwezo wa kuonesha mzunguko wa jalada kwa uwazi.
Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kuzinduliwa kwa mfumo huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuboresha mifumo ya utendaji kazi Serikalini.