Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE: USHINDANI WA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA NI JAMBO LISILOEPUKIKA KWA SASA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amesema suala la ushindani katika upatikanaji wa ajira katika Utumishi wa Umma ni jambo lisiloepukika kutokana na idadi kubwa ya wasomi iliyopo kwa sasa
Amesema dhamira hiyo ya kuhakikisha waombaji kazi wote wanafanya usaili kunasaidia kuwapata watumishi wenye sifa stahiki katika utumishi wa umma na kuondoa dhana ya upendeleo iliyokuwa imejengeka miongoni mwa watu
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo alipotembelea kituo cha usaili wa kada ya Ualimu Mkoani Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo, ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 inayoelekeza kuwa ajira katika utumishi wa umma zipatikane kwa ushindani
"Hakuna palipoandikwa kuwa watu wote waliosoma wataajiriwa na Serikali ndio maana ajira za serikali ni za ushindani kwani waliosoma ni wengi lakini nafasi ni chache.
Amesema Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma mara baada ya kutangaza kazi za Ualimu, waombaji 201,707 walijitokeza kuomba lakini baada ya mchujo kutokana na baadhi kutokukidhi vigezo ikiwemo kutokuweka baadhi ya vyeti kama ilivyoelekezwa walichujwa hadi kufikia waombaji 107,746
Hata hivyo, Mhe.Simbachawene ametumia fursa hiyo kuwasihi waombaji kazi kuhakikisha wanaweka vyeti vyao vinavyotakiwa ili kuepuka na mchujo katika hatua za awali.
Usaili wa kada ya Ualimu unaendelea katika vituo mbalimbali nchi nzima na utakamilika Februari 24 Mwaka huu.