Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE: SERIKALI YATENGA BIL. 11 MABORESHO YA HOSPITALI YA AMANA
![](https://www.utumishi.go.tz/uploads/news/e910a7ff7d1ad0240c020cf52298b035.jpeg)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Tanzania imepokea Dola milioni 14.5 kutoka Ubalozi wa Korea Kusini, sawa na shilingi bilioni 38 ambazo zitagawanywa katika hospitali tatu ikiwemo Hospitali ya Rufaa Amana ambayo itapata kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuboresha ujenzi wa majengo ya huduma ya mama na mtoto.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akimwakilisha Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika harambee maalumu ya kuchangia ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajazito iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi Milimani City, Dar es Salaam.
Mhe. Simbachawene amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika hospitali za Amana, Temeke pamoja na Mbagala katika kuhakikisha wajawazito na watoto njiti wanapata huduma bora na hivyo vifo kuchangia katika kupunguza vifo wakati wa kujifungua.
Aidha amewashukuru wadau wote kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kwa kujitoa katika harambee hiyo maalumu na kuwasihi watoe kwa moyo kwani hospitali ya Amana ni kubwa na lazima yafanyike makubwa.
“Mimi ni mwana Amana, watoto wangu wawili wamezaliwa Amana, maisha yangu ya Dar es Salaam ni Vingunguti, kwa hiyo naifahamu Dar es Salaam vizuri pia naifahamu Ilala na Amana ndiyo hospitali yangu,” ameongeza Waziri Simbachawene
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema katika harambee ya kuchangia ukabarati na ijenzi wa majengo ya Watoto njiti na wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Amana kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kimepatikana kutoka kwa wadau mbalimbali waliojitokeza kuchangia.
Ametoa wito kwa wadau na Marafiki wa Amana kuendelea kujitoa kwa hali na mali ili fedha zitokazopatikana ziweze kukamilisha majengo hayo
Amewahakikisha wadau hao kuwa fedha itakayopatikana itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio vinginevyo