Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE: SERIKALI YA TANZANIA KUHAKIKISHA UCHAGUZI MKUU UNAKUWA HURU, WA HAKI NA WA KUAMINIKA  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu unakuwa huru, wa haki, uwazi na kuaminika.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Alhamisi  Mei 8, 2025 jijini Arusha wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wanasheria unaofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo.

Amesema katika kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, unakuwa wa amani, huru, wa haki na unaoaminika, Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kufanya Mapitio ya Sheria za Uchaguzi, Kuimarisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kutoa Elimu ya Mpiga Kura, Kuhakikisha Usalama na Amani, Kujenga Maridhiano ya Kisiasa,  Kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura; kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi mkuu unaofuata.

 

Amesema uchaguzi ni suala la Kikatiba na Kisheria huku akisisitiza kuwa Chama Cha Wanasheria Tanganyika  (TLS) ni  Wakili wa Wananchi hivyo kina dhamana kwa Taifa kusaidia wananchi kuelewa umuhimu wa uchaguzi na kuwa ushiriki wa kila Mtanzania katika uchaguzi ni suala la kikatiba kupitia Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ni utekelezaji wa Ibara ya 8 ya Katiba kwa kuwa mamlaka ya utawala yanatoka kwa wananchi.  

 

“TLS ni chombo cha Umma hivyo Mawakili mna nafasi ya kipekee ya kuhakikisha wananchi wanapata haki ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu huku kukiwa na mazingira bora kwa pande zote” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Amesema TLS imekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha haki, kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, na kufuatilia mienendo ya uchaguzi na kuongeza kuwa Serikali inatambua juhudi zao katika kutoa elimu ya mpiga kura na kushiriki katika uangalizi wa kisheria wakati wa chaguzi”.

Ametoa wito kwa TLS kuendelea kushirikiana na Serikali, hasa kwa kutoa mapendekezo ya kisheria kuhusu marekebisho ya sheria za uchaguzi, kutathmini utekelezaji wa sheria hizo, na kuhakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika kwa njia ya haki.

Kwa upande wake, Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mhe. Boniphace Mwabukusi amesema misingi ya utawala bora katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu ni muhimu ikazingatiwa ili Taifa liendelee kubaki moja kabla na baada ya uchaguzi Mkuu

 

Amesema kuwa Watanzania wanahitaji haki na thamani ya kura yao kwa kuchagua viongozi wanaowataka na sio vinginevyo 

"Wakati mwingine TLS imekuwa ikikemea na kuonesha wapi pa kurekebishwa na hili lisichukuliwe kama jambo baya bali ndo wajibu wetu na sisi hatuna maslahi binafsi" Amesisitiza Mhe.Mwabukusi

 

"Tunafanya hili kwa dhamira ya dhati ili kuhakikisha maslahi kwa umma ndo kipaumbele chetu.’’ Amesisitiza