Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE: SERIKALI INATAMBUA NA KUTHAMINI MCHANGO WA WA KADA YA MENEJIMENTI YA KUMBUKUMBU NYARAKA 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali inatambua na kuthamini  mchango wa  kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka katika ustawi wa utumishi wa umma huku akiahidi wakati wote  Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora itaendelea  kutoa ushikiano kwa kada hiyo ili kuendelea kufanikisha masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Mhe Simbachawene ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka ( TRAMPA ) kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa kwa ajili ya  kufungua Mkutano huo.

Amesema mikutano hiyo ya Kitaaluma imekuwa ikileta tija kwa Wanataaluma hao  kwani mbali ya kupata maarifa bali wamekuwa wakibadilishana mawazo ya namna bora  ya kuboresha utendaji kazi wao 

Ameongeza kuwa " Mikutano hii ni muhimu kwao   kwani imekuwa ikitoa dira kwa Wanataaluma  namna ya kutumia mifumo ya TEHAMA katika kazi zao za kila siku badala ya utaratibu wa ubebaji wa mafaili uliokuwa ukifanyika hapo awali " 

Aidha, Mhe.Simbachawene amewataka Wanachama hao kufanya kazi kwa bidii na kujiongezea maarifa ili kuendana na mabadiliko ya TEHAMA  yanatokea katika utendaji kazi wao wa kila siku huku akiwataka Waajiri kuhakikisha wanakuwa msaada katika kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

Wakati huo huo, Waziri Simbachawene amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa ajira kwa watumishi wa umma wakiwamo watunza kumbukumbu. Katika mwaka 2024-2025 kada hii tu ajira mpya zilizotolewa ni 965 waliopandishwa cheo ni 1,237, kuwabadilishia kada watumishi 59 (Recategorization) pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kiasi cha shilingi milioni 204.6

Katika hatua nyingine,  Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora imeahidi kuchangia  kiasi cha Shilingi Mil.10 ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa Kituo cha Maarifa kitakachokuwa na masijala ya mfano, kumbi za mikutano pamoja na ofisi za TRAMPA kinachotarajiwa kujengwa jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kutoa ahadi hiyo, Mhe.Simbachawene amesema  kimsingi kazi hiyo ya ujenzi wa Kituo Maalum cha Maarifa cha TRAMPA kilipaswa kujengwa  na Serikali hivyo wao kama Ofisi yenye dhamana ya kusimamia Watumishi wa Kada hiyo imeamua kuwa mstari wa mbele kuchangia kiasi hicho 

Naye, Katibu Mkuu, UTUMISHI, BwJuma Mkomi ameahidi kutoa Sh.milioni 10 kwa niaba ya timu Menejimenti ya Ofisi hiyo ili kuhakikisha maono ya kujenga Kituo hicho cha Maarifa yanatimia.

Awali, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota Mrope amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta mbalimbali iliwemo katika kada ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka.

Rais Dkt. Samia amekuwa mwana TRAMPA namba moja, amepigania maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo sisi  mwana TRAMPA, ametoa ajira nyingi katika kipindi kifupi ikiwemo kwa  wanataaluma wa kada hii ya Menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka, amefanyia kazi changamoto zetu kwa kiasi kikubwa.