Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE: e-GA IMEFANIKIWA KUJENGA  MFUMO WA KUBADILISHANA TAARIFA  KWENYE TAASISI ZA SERIKALI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Mhe. George Simbachawene amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)  imefanikiwa kujenga mfumo ambao unawezesha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini kuunganishwa, kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

Amesema  kwa sasa mifumo 218 kutoka kwenye Taasisi  zipatazo 181 imeunganishwa na inasomana.

Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kuitikia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka  mifumo inayotumika kwenye Taasisi za Umma kusomana ili kurahisisha utendaji kazi Serikalini na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo Februari 11, 2025 jijini Arusha wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Mpango  akifungua Kikao kazi cha 5 cha Serikali Mtandao kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

 

Amesema e-GA itaendelea kusimamia uunganishwaji wa mifumo ya kubadilishana taarifa kulingana na mahitaji yaliyopo.

 

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema  kikao kazi hicho kilimualika Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo  la kumshukuru kwa mchango wake mkubwa pamoja  na kutoa hamasa katika matumizi ya TEHAMA kwani ndiyo chachu iliyopelekea mafanikio hayo yanayoonekana kitaifa na kimataifa.

 

Katika hatua nyingine,  Mhe. Simbachawene amesema Tanzania imeweza kutambulika Duniani kwa kushika nafasi ya pili  katika Bara la Afrika na kuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwenye ripoti ya utafiti wa ukomavu wa matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi kulingana na ripoti  ya  Benki ya  Dunia.

Ameongeza kuwa  “Kama nchi tumepiga hatua kubwa  katika uwezo wa kujenga miundombinu ya kuhifadhi taarifa na kuweza kubadilisha utendaji kazi wetu kwenda kwa njia ya mtandao"

Awali Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka  ya Serikali Mtandao, ( e-GA)  Mhandisi Benedict Ndomba alisema e-Ga imesaidia  matumizi sahihi na ya uhakika kwenye Taasisi za Serikali kwa kuwezesha utoaji wa  huduma kwa wakati. 

Amesema e-GA imeleta mapinduzi makubwa katika matumizi ya TEHAMA Serikalini kwani imechagiza utendaji kazi wa Serikali na kuongeza ufanisi kwenye Taasisi mbalimbali  ikiwemo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ( NIDA)  Mifumo ya fedha ya Benki Kuu ( BOT)  pamoja na Mfumo wa Manunuzi ( Nest)  

Naye Katibu Mkuu-IKULU, Bw. Mululi Mahendeka amesema e-GA imeleta mageuzi makubwa kwenye Taasisi za Serikali  kwa kuboresha utendaji kazi wa kila siku na utoaji wa huduma kwa jamii kuwa rahisi na wa haraka 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala,  Katiba na  Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema Bunge ni moja ya wanufaika wakubwa wa gunduzi zilizofanywa na e-Ga. 

Amesema Serikali imepiga hatua kubwa kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo yameleta tija na ufanisi wa hali ya juu latika utoaji wa huduma bora za haraka na za uhakika kwa wananchi.

"Tunaipongeza sana e-GA kwa bunifu wanazoendelea kufanya, kama Bunge tunataka mifumo yote ya kidigitali inayotumika na Serikali isimamiwe na idhibitiwe na e-GA ili kulinda taarifa za Serikali.