Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE AZITAKA TAASISI ZA UMMA KUTUMIA MIFUMO YA KIDIJITI KURAHISISHA UTOAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amezitaka Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinatumia mifumo katika kuwahudumia wananchi kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma bora, urahisi na haraka.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati wa akifungua Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yenye kaulimbiu ya "Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji"
Amesema Serikali imejenga mifumo mingi ikiwemo wa kufuatilia utendaji kazi wa watumishi ambao umeondoa ubabaishaji.
Kadhalika, Waziri Simbachawene amewataka wananchi kutumia mfumo wa e-malalamiko na e-mrejesho ili kuweza kuainisha changamoto ambazo Serikali itazifanyia kazi kwa wakati na kuboresha utoaji wa huduma.
"Nizielekeze Taasisi zote za Umma kutumia mifumo iliyojengwa ili kurahisisha utoaji wa huduma bora, kwa haraka na kwa urahisi."
Kwa upande wake Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma imeshirikisha Wizara 23, Mikoa 5, Halmashauri 3 na taasisi za umma 101 zimeshiriki.
Amesema kupitia maadhimisho hayo wananchi wanapata fursa ya kuhudumiwa moja kwa moja, kufahamu majukumu ya Taasisi na Wizara kupata mrejesho ili kuboresha utoaji wa huduma.
Katika hatua nyingine, Bw. Mkomi ametoa wito kwa wananchi, watumishi wa umma na wadau mbalimbali kuendelea kutembelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma ambapo Maadhimisho hayo yataendelea hadi Juni 27 mwaka huu.