Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE AWASISITIZA WATUMISHI WA OFISI YAKE KUTOA HUDUMA ZENYE VIWANGO KWA WANANCHI


Na Lusungu Helela-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Watumishi wa Ofisi yake kutoa huduma bora kwa wananchi kwa haraka na ufanisi, huku akisisitiza ubora wa huduma hizo uendane na uzuri wa jengo jipya ambalo Ofisi hiyo imehamia hivi karibuni.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo jana jioni mara baada ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi hiyo na kuwakutanisha Watumishi wote wa Ofisi hiyo wakiwemo baadhi ya viongozi kutoka Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo,  ikiwa ni hatua muhimu ya kujumuika kwa pamoja mara baada ya  kuhamia katika jengo jipya lililopo Mtaa wa Utumishi, Mji wa  Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

 

Amesema anatamani kuona wananchi na watumishi wanaohudumiwa katika jengo hilo jipya wanafurahia huduma wanazozipata kwani kitendo cha Watumishi kuhamia katika jengo hilo jipya kwa sasa kuna utulivu wa akili.

 

“Sasa watumishi wote tupo katika jengo moja, sitegemei kusikia visingizio vya hapa na pale kuwa jalada fulani halipo Mtumba bali liko Ofisi za UDOM kule ambako baadhi ya watumishi walikuwa wakifanya kazi, tufanye kazi,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

 

Amesema kitendo cha Watumishi kuhamia katika jengo moja tofauti na ilivyokuwa mwanzo ni muhimu sasa kwa Watumishi wa Ofisi yake kushirikiana katika kufanya kazi ili kuhakikisha wateja wanaridhika na huduma wanazozipata.

 

"Serikali imejenga jengo zuri mno, hii kwenu ni motisha kubwa, hivyo hakikisheni huduma mnazozitoa ziwe za viwango vya hali ya juu ili kuendana na thamani ya jengo" amesema Mhe. Simbachawene.

 

Aidha, Mhe. Simbachawene ameiagiza Ofisi hiyo kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi kwa pamoja lengo likiwa ni kulinda afya pamoja na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ili kuweza kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

 

"Kwa sasa tupo jengo moja, naagiza utaratibu uandaliwe wa kufanya mazoezi kwa pamoja ili kulinda afya zetu na kuwahudumia wananchi ipasavyo" amesema Mhe.Simbachawene

 

Awali, Katibu Mkuu UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi alimshukuru Waziri Simbachawene kwa wazo la kuandaa Iftar hiyo huku akiwataka Watumishi wa Ofisi yake kushirikiana katika kuwahudumia wananchi.

 

"Mtaungana nami, leo ni siku muhimu sana ambapo Waislamu mpo katika mfungo wa Ramadhani huku Wakristo mkiwa katika mfungo wa Kwaresma, tumekutana hapa ili kufuturu pamoja kuonyesha ishara ya upendo na ushirikiano," Bw. Mkomi amesisitiza.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la shukrani kwa Waziri Simbachawene amemuahidi kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatafanyiwa kazi chini ya uongozi wa Katibu Mkuu ikiwemo utamaduni wa namna hiyo wa kukutana kwa pamoja.