Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA WITO KWA TAASISI ZA SERIKALI KUHIFADHI KUMBUKUMBU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utwala Bora, Mhe.George Simbachawene ametoa wito kwa Taasisi za Umma zenye kumbukumbu nyeti kuhusu sekta zao kuitumia Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuzihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Idara hiyo iliyopo Jijini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kuzungumza na Watumishi na kuhimiza uwajibikaji.
Hata hivyo, Mhe.Simbachawene ameitaka Idara hiyo kuendelea kutoa elimu kwa Taasisi za Umma kuhusu umuhimu wa kuzihifadhi Nyaraka walizonazo kwa rejea ya baadae.
" Leo nimejifunza mambo mengi hususani ukombozi wa Bara la Afrika na Makabila ya Tanzania, hakika Idara imesheheni historia lukuki" ameeleza Mhe.Simbachawene
Aidha, ameongeza kuwa kumbukumbu na nyaraka za Serikali ni lazima zipewe kipaumbele kwa kuhifadhiwa sehemu salama hivyo ni muhimu kutenga bajeti ya kutekeleza jukumu hilo mahususi.
Kutokana na umuhimu wa Idara hii, amewataka watumishi wa Idara hiyo kujiepusha na tabia ya kuvujisha siri kwa kuwa baadhi ya Nyaraka wanazozihifadhi zimebeba siri kubwa ya nchi.