Habari
WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA MAAGIZO TISA KWA WAKUU WA TAASISI ZA UMMA NCHINI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametoa maelekezo tisa kwa lengo la kuboresha Utumishi wa Umma ikiwamo kuwataka Wakuu wa Taasisi za Umma kuchukua hatua stahiki pale maadili yanapothibitika kuwa yamekiukwa na watumishi.
Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Machi 3, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi kati yake na Wakuu wa Taasisi za Umma.
Amesema ni vyema Wakuu wa Taasisi za Umma kuendelea kusimamia utawala na rasilimaliwatu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika Utumishi wa Umma.
Pia, Mhe. Simbachawene amewataka Wakuu hao wa Taasisi kuhakikisha Ofisi zao zinajiunga na kutumia kikamilifu mifumo ya kidijiti ya kiutumishi iliyosanifiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Amesema taarifa za Watumishi zilizopo katika Mfumo Jumuishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-Watumishi) zisafishwe kwa ajili ya kuwezesha kufanyika kwa maamuzi sahihi ya masuala mbalimbali ya kiutumishi.
Mhe. Simbachawerne amewasisitiza Wakuu hao wa Taasisi kuacha kuwasilisha au kupitisha nakala ngumu za barua za maombi ya masuala ya kiutumishi ambayo kwa sasa yanashughulikiwa kupitia mifumo ya kidijiti.
Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga nafasi za ajira mpya kwa kuzingatia maelekezo ya mwongozo wa maandalizi ya ikama na bajeti hususan kwenye maeneo ya rasilimaliwatu yenye upungufu mkubwa na ambayo ni kipaumbele cha Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
‘’Watumishi wanaopangiwa katika vituo vyenu vya kazi au waliohamishiwa katika taasisi zenu muwapokee kwa mujibu wa maelekezo pamoja na kuwachukulia hatua stahiki watumishi wenye utendaji kazi usioridhisha kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.” Amesema Mhe. Simbachawene
Ameagiza nafasi za uongozi zilizowazi katika sehemu za kazi zijazwe kwa kuzingatia Sheria, Kanuni naTtaratibu zilizopo.
“Tekelezeni jukumu la kuwaandaa watumishi wenu na mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kujitokeza kwa kuwaandalia mafunzo yenye kukidhi matarajio ya nchi yetu pamoja na mazingira yanayotuzunguka ili wakabiliane na mabadiliko yanayoendelea kwa kasi duniani.” Ameongeza
Pia amewaelekeza Wakuu hao wa Taasisi za Umma kusimamia kwa vitendo, maadili katika sehemu za kazi za umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa siri za Serikali zinatunzwa vizuri.
“Mnaelekezwa kuchukua hatua stahiki pale maadili yanapothibitika kuwa yamekiukwa na Watumishi walio chini yenu.” Amesema Mhe. Simbachawene
Amehimiza uimarishaji wa usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba ya huduma kwa mteja katika Taasisi na kutoa taarifa za utekelezaji wa mkataba hiyo kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Pia amewataka kuziba pengo la upungufu wa watumishi kwa kutoa ajira za mikataba kwa kuzingatia Waraka wa Katibu Mkuu, UTUMISHI kuhusu kujitolea katika Utumishi wa Umma.
“Utaratibu huu utasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa fani mbalimbali.”
Mhe. Simbachawene pia amewataka wakuu wa Taasisi za Umma kutoa nafasi za Mafunzo kwa Vitendo ili kusaidia kuandaa rasilimaliwatu ya baadaye yenye weledi na uwezo wa kutekeleza majukumu ya Serikali.