Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE ASIFU USHIRIKIANO WA SEKRETARIETI YA MAADILI  YA VIONGOZI WA UMMA NA IAA KUKUZA MAADILI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA)  kwa kuanzisha ushirikiano katika mafunzo ambayo yatalenga kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa maadili na uwajibikaji wa viongozi wa umma yanakuwa dhahiri na yanaimarishwa kupitia elimu na utafiti. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Simbachawene amesema kuwa Mpango wa Taifa dhidi ya Rushwa na Kukuza Uadilifu ni dhamira ya dhati  ya Serikali ya kuhakikisha kuwa jamii inayojengwa inakuwa  na  maadili, uwajibikaji, na uwazi katika kuwahudumia wananchi.

Aidha, Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza mara kwa mara kuwa "Mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kuwa kazi ya mtu mmoja au taasisi moja; ni jukumu letu sote kama Taifa. Hivyo,  nazipongeza kwa dhati taasisi hizi mbili". 

Awali,  Mkuu wa Chuo cha IAA  Prof. Eliamani Sedoyeka  alisema , elimu bila maadili ni hatari, na maadili bila elimu ni bure. 

Amefafanua kuwa elimu ya kitaaluma na maadili thabiti katika uongozi ni jambo lisiloepukika . ‘‘Taasisi za elimu ya juu zina wajibu wa kuhakikisha kuwa wanaowazalisha wanakuwa si tu wataalamu wa fani zao, bali pia viongozi wenye maadili mema na wenye kuzingatia misingi ya utawala bora’’

Amesema makubaliano hayo na Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa Umma yamejikita katika kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii. 

Pia, Prof. Sedoyeka, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuweka msisitizo katika kukuza maadili ya viongozi wa umma huku akisema kuwa anaamini kwa pamoja, wataweza kujenga Tanzania yenye utawala bora na maendeleo endelevu.

Naye Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesii amesema maadili na uongozi bora ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo taasisi za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa.

Mhe. Jaji (Mst) Mwangesi amesisitiza kuwa, kupitia ushirikiano huo wataweza kujenga mfumo imara wa maadili unaozingatia misingi ya haki, usawa, na utawala bora na sio tu kwa viongozi wa umma bali kwa watumishi wa umma wote kwani hata hao viongozi ni wale wanaotokea kwenye Utumishi wa Umma.