Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TAKUKURU KUWADHIBITI WACHEZEAJI RASILIMALI ZA NCHI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kudhibiti mianya ya rushwa katika fedha za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali nchini ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

                    

Ametoa kauli hiyo  leo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi za TAKUKURU mkoani Iringa ambapo amemtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo  ifikapo mwezi Juni mwaka huu kama ilivyopangwa ili watumishi wa taasisi hiyo waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri. 

 

“Tukawe watu wa kupekenyua pekenyua kwenye miradi hii inayotekelezwa na serikali kwani kuna watu wanatumia vibaya fedha za serikali, penyeni huko kuwadhibiti ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati na kwa viwango kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Mhe. Simbachwene

 

Amefafanua kuwa TAKUKURU inatakiwa kuhakikisha inasimamia na kudhibiti fedha zisipotee lakini bila kuathiri maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini.

 

"Palipo na shilingi ya Mama Samia waambieni TAKUKURU tupo ila katika kufanya haya tusikwamishe maendeleo" amesisitiza Mhe. Simbachawene.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene ameitaka Taasisi hiyo kuwachukulia hatua wale wote wanaokwamisha shughuli za maendeleo na hivyo kukwamisha utendaji wa Rais Mhe. Dkt.  Samia suluhu Hassan.

 

"Dhibitini mianya ya kuchezea rasilimali za nchi ikiwemo fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sehemu ambako fedha imesimamiwa vizuri matokeo mazuri yameonekana, naomba niwasihi kuendelea kuwadhibiti ipasavyo wachezea fedha za maendeleo" amesema Mhe. Simbachawene.

 

Ameongeza kuwa anataka kuona TAKUKURU ikichukua hatua kwa wale wote wanaokwamisha nia nzuri ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kama hatua hizo hazichukuliwi basi miradi mizuri iliyotekelezwa ionekane ili wananchi wazidi kuwa na imani na serikali yao.

 

Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni amesema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja hadi kukamilika kwake mwezi Juni mwaka huu utagharimu zaidi ya shilingi billioni 1.4.

 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo huku akiipongeza TAKUKURU kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia fedha za serikali zisipotee kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watu.