Habari
WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA ATAKA MPANGO MKAKATI WA MATUMIZI WA MIFUMO YA KIDIGITALI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi za Umma kuweka mipango madhubuti ya kutumia mifumo ya kidijitali ambayo italeta mageuzi ya kiutendaji na kuifanya Tanzania kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda yanayotumia TEHAMA.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Juni 23 , 2024 jijni Dodoma katika viwanja vya Chinangali Park wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na Uzinduzi wa mifumo ya kidijitali iliyosanifiwa na kujengwa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Amezitaka Taasisi hizo kufuatilia na kuhimiza matumizi ya mifumo hiyo kwa Watumishi wanaowaongoza.
Amesema uzinduzi wa mifumo hiyo ya kidijitali ni utelelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo Serikali itaweza kuwahudumia wananchi kwa uwazi na kwa haraka zaidi.
Ameitaja mifumo iliyozinduliwa kuwa ni HR Assesment, PEPMIS na PIPMIS, e-Watumishi (HCMIS) pamoja na e-Mrejesho.
Amesema mifumo hiyo ikitumika ipasavyo itasaidia kuwabaini Watumishi mahiri na watumishi wazembe pamoja na kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utumishi wa umma.
"Mifumo hii ikitumiwa kama ilivyokusudiwa itasaidia kuwabana Watumishi wazembe na hivyo kuongeza uwazi uwajibikaji na ufanisi katika kuwahudumia wananchi " amesisitiza Mhe.Majaliwa
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewapongeza vijana wazawa kwa ubunifu wa kusanifu mifumo hiyo huku akiutaja mfumo wa e-Mrejesho uliotambulika kimataifa kutokana na ubora wake.
Akizungumzia Wiki ya Utumishi wa Umma amesema moja ya lengo lake ni kuhimiza uwajibikaji, uwazi, uadilifu pamoja na utoaji huduma bora kwa wananchi
"Hongereni sana Taasisi za Umma kwa utayari wenu wa kutoa huduma kwa wananchi kuanzia Juni 16 hadi leo hii siku ya Kilele" amesisiiza Waziri Mkuu.
Amesema kitendo cha kufanyika kwa maonesho hayo ni dalili tosha kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kutoa huduma bora za papo kwa hapo kwa wananchi pasipo wananchi kulazimika kuzifuata huduma hizo maofisini.
Kwa upade wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ys Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema matumizi ya TEHAMA katika Utumishi wa Umma yameondoa usumbufu, rushwa pamoja na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.
Amesema mifumo hiyo imesanifiwa na kujengwa na wazawa ukiwemo mfumo wa e-Watumishi (HCMIS) ambao una uwezo wa kuhifadhi taarifa za watumishi wa umma kuanzia siku aliyoajiriwa hadi siku ya kustaafu.
Amesema mfumo wa upimaji wa utendaji kazi kwa watumishi na taasisi PEPMIS na PIPMS umesaidia kuondoa upendeleo na uonevu na unahamasisha utendaji kazi miongoni mwa watumishi.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bw.J uma Mkomi amesema matumizi wa Mifumo ya Utendaji Kazi ikiwemo PEPMIS na PIPMIS imeonekana kuwa ni kikwazo kwa baadhi ya Watumishi kwa sababu Watumishi wengi hawapendi kubanwa
Bw. Mkomi amesema mtumishi yeyote ambaye hatojaza majukumu yake kwenye mfumo huo hatopata ruhusa ya kuhama wala kwenda masomoni pamoja na kutopanda cheo
Katika hatua nyingine Bw. Mkomi amesema Mfumo wa e-mkopo umewarahisishia Watumishi wa Umma kupata mkopo kwa haraka na pia mfumo huo hautoi fursa kwa Watumishi kukopa benki nyingine endapo Mtumishi atakuwa na mkopo katika benki nyingine.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala Bora, Mhe. Frolent Kyombo ameipongeza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa usanifu na kujenga mifumo hiyo ya Kidijitali kwani imesaidia kupunguza usumbufu na gharama kwa watumishi wa Umma wa kufuatilia huduma Dodoma.