Habari
WAZIRI KIKWETE AISISITIZA TAKUKURU KUJIRIDHISHA NA USHAHIDI WA KESI ZA WATUHUMIWA KABLA YA KUZIPELEKA MAHAKAMANI
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 20, 2026, alipokuwa akizungumza na watumishi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Ofisi yake na kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.
Amesema katika miaka ya hivi karibuni TAKUKURU imeshindwa kufanikiwa kwenye baadhi ya kesi na hii sio kwamba inaonewa, yawezekana kuna sehemu katika ushahidi hawajajipanga vizuri.
“Nawaombeni sana Maafisa Uchunguzi wetu tujiridhishe, msitumike katika kuwapotezea watu muda, ni muhimu tukajiridhisha juu ya ushahidi wa kesi zetu na utayari wa kupeleka kesi Mahakamani. Haipendezi kesi kuendeshwa kwa zaidi ya miezi mitano, halafu mwisho mtuhumiwa ashinde kwa kukosekana kwa ushahidi wa kutosha,” amesema.
Ameongeza kuwa watumishi wa taasisi hiyo wanapaswa kuhakikisha haki inatendeka bila kumuonea haya mtu yeyote wala kupindisha Sheria, Taratibu na Kanuni katika kila hatua ya uchunguzi.
Aidha, ameipongeza Taasisi hiyo kwani pamoja na kutofanikiwa katika baadhi ya kesi kwa kukosa ushahidi lakini amewapongeza kwa kesi walizoshinda ambazo zilikuwa na ushahidi wa kutosha huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Amesema takwimu za mwaka uliopita zinaonyesha TAKUKURU imeshinda zaidi ya asilimia 70 ya kesi za rushwa ilizofikisha mahakamani.
Awali , Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila, amesema taasisi hiyo itaendelea kutanguliza uzalendo, weledi, uwajibikaji na haki katika kushughulikia kesi za rushwa na uhujumu uchumi.
Chalamila amesema TAKUKURU ina Kitengo cha Maadili ya Watumishi kinachoongozwa na Mkurugenzi na moja ya majukumu yake ya msingi ni kuchunguza watumishi wa taasisi hiyo ili kuhakikisha wanakuwa mfano bora kwa jamii.
“Tuna Kitengo cha Maadili ya Watumishi wa TAKUKURU na kinaongozwa na Mkurugenzi. Moja ya jukumu lake la msingi ni kuwachunguza watumishi ili tuwe mfano na kioo bora kwa jamii,” alisema
