Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAZIRI KIKWETE AAHIDI USHIRIKIANO KWA WATUMISHI WA WAKALA YA NDEGE ZA SERIKALI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete ameipongeza Bodi, Menejimenti na Watumishi wa Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) kwa kuongoza na kusimamia Ndege za Serikali kwa weledi na  ufanisi mkubwa.

Waziri Kikwete amesema hayo Desemba 12, 2025 jijini Dar es salaam wakati alipotembelea ofisi ya Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) kwa lengo la kujitambulisha.
“Ninaipongeza Bodi kwa kuendelea kuwa washauri wazuri na kufanya uendelevu wa Wakala, binafsi ninaridhika na utendaji kazi wake. Pia Nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wote kwa ustadi wenu mkubwa wa kusimamia Ndege za Serikali, mimi na Naibu Waziri wa ofisi yangu Mhe. Regina Qwaray tunawahakikishia ushirikiano wa dhati wakati wote wa uongozi wetu” alisema Mhe. Kikwete.

Aidha, Mhe. Kikwete amewapongeza kwa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi ambao unaonekana kuridhisha viongozi wanawahudumia. Hivyo, ametoa rai pia kwa watumishi hao kumpa ushirikiano Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray kwa kuwa anamfahamu uwezo wake katika kazi na atasaidia kuongeza ufanisi mara dufu.

Vile vile Mhe. Kikwete amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuongoza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo TGFA ni moja ya taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ameahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya taasisi hiyo muhimu katika Taifa.

“Leo tumekuja kujitambulisha ili tupate kufahamiana kwa kuwa sisi ndio tutafanya kazi pamoja, naomba tuendelee kuwa na ari ile ile ya kufanya kazi kwa ushirikiano ili tuweze kufanikiwa” alisema Mhe. Qwaray.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali Capt. Budodi Nicholaus Budodi alisema kuwa Wakala inaendelea vizuri kusimamia miradi mbalimbali inayoendelea katika ofisi hiyo.

Vile vile, kwa niaba ya taasisi ameahidi kuendelea kuwa wasikivu katika maelekezo wanapata  kutoka kwa viongozi na kutekeleza kwa wakati na kwa ufanisi.