Habari
WATUMISHI WAPATIWA ELIMU KUHUSU HATI YA KUSAFIRI, NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI ASISITIZA UMUHIMU WA MAFUNZO YA MARA KWA MARA KUJENGA UTUMISHI WA UMMA WENYE WELEDI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, amesisitiza umuhimu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa Umma, akieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuongeza maarifa na ujuzi, kujenga uwezo na kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.
Bi. Lwangili ameyasema hayo leo wakati akihitimisha mafunzo yaliyohusu uelewa na maarifa ya watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu hati ya kusafiri, ikiwemo taratibu za kuomba, kupata na kutumia hati hiyo kwa usahihi yaliyofanyika leo Agosti 17, 2026, katika eneo la wazi la Ofisi hiyo jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, Naibu Katibu Mkuu Lwangili amesema kuwa kuendelea kuwawezesha watumishi kupata elimu na ujuzi katika maeneo mbalimbali ni sehemu ya juhudi za Serikali za kujenga Utumishi wa Umma wenye weledi, ufanisi na unaozingatia viwango vya ubora katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Awali akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mrakibu Msaidizi wa Uhamiaji, Bw. Segere Zonzo, amewakumbusha watumishi umuhimu wa kuwa na uelewa sahihi wa taratibu za kupata na kutumia hati ya kusafiri.
Bw. Zonzo amesema kuwa uelewa huo utawawezesha watumishi kuzingatia taratibu na kutumia hati hiyo kwa usahihi, hivyo kurahisisha safari zao za nje ya nchi, hususan wanaposafiri kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kikazi au shughuli binafsi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utaratibu wa Ofisi ya Rais – Utumishi wa kuwawezesha watumishi kuendelea kujifunza na kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Utumishi wa Umma, sambamba na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
