Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WAFUNDWA KUHUSU AFYA YA AKILI


Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili,  Dkt. Garvin Kweka, amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  kuweka uwiano sawa katika maisha ya kazini na binafsi  ili kuepuka tatizo la afya ya akili.

Dkt. Kweka ametoa wito huo leo, wakati akitoa elimukwa Watumishi wa Ofisi hiyo , kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo la msongo wa mawazo katika maisha ya kazini na binafsi, ikiwa ni muendelezo ya mafunzo ambayo hufanyika kila jumatatu ya wiki nyakati za asubuhi katika Ofisi hiyo Mtumba Jijini, Dodoma

Amesema Watumishi wa Umma walio wengi wamekuwa wakiamini uwepo wao katika Ofisi ni muhimu kana kwamba bila wao hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika.

Amefafanua kuwa hali hiyo imefanya baadhi ya Watumishi hao kujikuta wakitumia muda mwingi kukaa maofisini na hivyo kupelekea kukosa uwiano baina ya maisha  binafsi na kazini,  hali inayopelekea kukosa muda wa kujichanganya na jamii yake.

Kufuatia hatua hiyo amewataka Watumishi hao kuwa na kiasi huku akiwasisitiza umuhimu wa kuchanganyana na jamii ili kuepukana na matatizo ambayo yanaweza kumpata endapo Mtumishi huyo atakuwa kivyake vyake muda wote. 

Amezitaja athari ambazo zinaweza kuwapata Watumishi hao kuwa ni pamoja na kujidhuru, kujiua na kuwa na hasira muda wote .

Hata hivyo,  Dkt.Kweka ametumia fursa hiyo kuwaonya Watumishi wa Umma  kuacha  tabia ya kukopa fedha kwa watu wengi ili kuepukana na tatizo la msongo wa mawazo.