Habari
WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUZINGATIA ELIMU YA USALAMA MAHALI PA KAZI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kutumia na kuzingatia elimu waliyopewa ya Usalama Mahali Pa Kazi kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana dharura mbalimbali ili kuondoa hofu ya kimwili na kiakili wanapokuwa wanawajibika katika maeneo yao ya kazi.
Bw. Daudi amesema hayo Machi 9, 2026 kwa Watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa kuhitimisha mafunzo ya uelewa wa Usalama Mahali pa Kazi yaliyofanyika Mtumba jijini Dodoma.
“Tumepatiwa elimu kuhusu Usalama Mahali pa Kazi, nitoe wito kwenu kuzingatia elimu hii kwa manufaa yetu sote ili kuondokana na hofu na kujenga uwajibikaji ulio bora tutakapokuwa tunatekeleza majukumu yetu katika maeneo ya kazi.” Bw. Daudi alisema.
Aidha, Bw. Daudi amewasisitiza watumishi hao kuzingatia suala la usafi wa mazingira wawapo katika maeneo yao ya kazi jambo ambalo litaongeza ufanisi katika utendajikazi kwani afya bora ni mtaji wa uwajibikaji utakaomwezesha mtumishi wa umma kutoa huduma bora itakayoongeza imani ya Wananchi kwa Serikali yao.
Vilevile, Bw. Daudi amempongeza Mkaguzi wa Mazingira ya Kazi kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Thadei Mwasamila kwa kutoa elimu hiyo kwa ufasaha kwani itasaidia kuongeza chachu ya utendajikazi kwa Waajiri na Watumishi.
Kwa upande wake, Bw. Mwasamila ametoa rai kwa waajiri na watumishi wa umma kuhakikisha wanazuia ajali mahali pa kazi ili kuwa na amani na kuondokana na hofu wanapokuwa wanatekeleza ma
