Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWA WAZALENDO ILI KUDUMISHA AMANI YA NCHI


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi hiyo, kuwa wazalendo wenye kuipenda nchi yao na rasilimali zilizopo ndani yake, ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya ugaidi na misimamo mikali inayotokana na ushawishi kutoka makundi yasiyofaa ambayo hupotosha umma na kuliingiza taifa katika vurugu na ukosefu wa amani.

Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 17/11/2025 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Ofisi anayoingoza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi hao yanayofanyika katika eneo maalum la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.

Aidha, Bw. Mkomi amewaasa Watumishi wa Umma kuendelea na uwajibikaji wenye kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya maadili inayowaongoza kama Uzalendo, Uaminifu na Mteja kwanza ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuondoa tofauti zilizopo kati ya serikali na wananchi kwa ustawi wa Taifa.

“Uwajibikaji na Amani ni vitu vinavyoenda sambamba katika kujenga jamii bora na imara, kila mtumishi anapotekeleza wajibu wake kwa dhati, hujenga  msingi mzuri wa amani kwa kuwa amani inahitaji ushirikiano wa pamoja katika kutatua changamoto za wananchi na hivyo jamii kuwa na uwezo wa kukua na kuwa na maendeleo endelevu” alisema Bw. Mkomi.

Awali akiwasilisha mafunzo hayo, Mwezeshaji ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Polisi Mkoa wa Dodoma ASP Christer Kayombo ameeleza sababu mbalimbali zinazopelekea kuwepo kwa vitendo vinavyosababisha ukosefu wa amani, ikiwa ni pamoja na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii, uvivu pamoja na watoto kukosa misingi bora ya malezi wakiwa wadogo na hivyo kukua na hali ya ujasiri wa kufanya maovu hayo bila hofu.

ASP Kayombo alihitimisha mafunzo hayo kwa kutoa wito kwa Watumishi wa Umma na wananchi wote kwa ujumla kuungana kwa sauti moja katika kuhamasisha amani ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya namna ya kuepuka vitendo viovu vitakavyosababisha uvunjifu wa amani na kukemea vitendo hivyo kwa maslahi ya Taifa.