Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA e-WATUMISHI KWA UADILIFU NA UWAJIBIKAJI


Wakuu wa Idara za Utumishi na Utawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Utumishi na Utawala wametakiwa kutumia Mfumo wa e-Watumishi kwa uadilifu, umakini na uwajibikaji ili kuboresha usimamizi wa rasilimaliwatu na mishahara katika Taasisi za Umma.

Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu – UTUMISHI, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango wa Ofisi hiyo Bw. Cosmas Ngangaji, Novemba 13, 2026 wakati akifunga mafunzo kuhusu mfumo huo yaliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspa jijini Dodoma.

Bw. Ngangaji amewataka washiriki kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi ikiwemo uzembe, matumizi ya lugha zisizofaa, kutoa taarifa za uongo na kufanya udanganyifu, akibainisha kuwa Mfumo Mpya wa e-Watumishi una uwezo wa kurekodi na kufuatilia shughuli zote zinazofanywa na watumiaji.

“Matumizi ya Mfumo Mpya wa e-Watumishi yanapaswa kuzingatia uadilifu  na uwajibikaji kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimaliwatu na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma,” amesema Bw. Ngangaji.

Aidha Bw. Ngangaji ameongeza kuwa mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma za kiutumishi kwani utawawezesha Maafisa Utumishi kutatua changamoto za watumishi katika Taasisi zao na kupunguza usumbufu wa kufuata huduma Ofisi ya Rais – UTUMISHI.

Katika mafunzo hayo, washiriki wamejengewa uwezo wa kutumia mfumo huo maeneo mbalimbali ikiwemo ya Ajira, Payroll, pamoja na kushughulikia masuala ya likizo, maadili na upandishaji vyeo kwa mserereko.