Habari
WATUMISHI WA UMMA WASISITIZWA KUZINGATIA MISINGI YA UADILIFU ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA UMMA

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewakumbusha Watumishi wa Umma kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari, kuwajibika katika kutoa huduma Bora kwa Umma kwa kuzingatia Misingi ya Uadilifu ili kuleta Ustawi kwa Wananchi.
Bw. Mkomi ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ushiriki wa Watumishi wa Umma katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja iliyoanza tarehe 06 hadi 10, Oktoba 2025 yenye Kaulimbiu isemayo “Dhamira Inayowezekana”.
Bw. Mkomi amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni simamizi katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja, hivyo imeendelea kuzingatia misingi yake ya maadili ikiwemo Uzalendo, Uadilifu, Ubora na Mteja Kwanza ikiwa ni sehemu ya kusimamia Dira ya Ofisi inayofanya kuwa na Utumishi wa Umma wenye ufanisi na uwajibikaji.
Vilevile Katibu Mkuu Mkomi amewataka Watumishi wa Umma kutumia Wiki ya Huduma kwa Mteja kuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji kwa kutoa huduma bora na kujenga taswira chanya kwenye ofisi kwa kuzingatia misingi ya maadili ili kupunguza malalamiko na kujenga imani ya Wananchi kwa Serikali yao.
“Ustawi wa Wananchi utapatikana kupitia utoaji wa huduma bora, unaozingatia maadili ya utendaji na maadili ya taaluma walizonazo Watumishi wa Umma hivyo, wanapotoa huduma wazingatie kuwa nadhifu, waaminifu, wakarimu, wenye heshima, wanaojali utu, kuepuka vitendo vya rushwa na kujali watu wanaowahudumia,” Bw. Mkomi amesisitiza.
Katika hatua nyingine alipokuwa akihitimisha hotuba yake, Katibu Mkuu Mkomi amesisitiza Watumishi wa Umma na Wananchi kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali utakaofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 ili kutumia haki yao ya Kikatiba ya kuchagua Viongozi watakaoiongoza nchi kwa ustawi wa Taifa