Habari
WATUMISHI WA UMMA, WANANCHI WAPEWA NYENZO YA KUWASILIANA NA SERIKALI
“Mfumo wa e-Mrejesho unalenga kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali na ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora ambayo inajali maslahi ya wengi, kuwa na uwazi, kupiga vita dhidi ya rushwa, kuleta haki na usawa na kuhimiza uwajibikaji”.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Janet Mishinga alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya Usimamizi Maadili imewahimiza Watumishi wa Umma na Wananchi kutumia Mfumo wa Kielektroni wa Kutuma, Kupokea na Kufuatilia Malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi Serikalini (e-Mrejesho) ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia mrejesho wa masuala mbalimbali ya kiutumishi na kuboresha huduma kwa umma.
Aidha Bi. Mishinga alifafanua kuwa, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mfumo wa e-Mrejesho una lengo la kubaini mafanikio na changamoto ili kuimarisha uadilifu katika kushughulikia mrejesho wa wananchi ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi katika kuhudumia wananchi.
Pia, alibainisha kuwa utaratibu wa kushughulikia mrejesho kuhusu mfumo huo unaongeza ushirikishwaji kwa watumishi wa umma na wananchi.
