Habari
WATUMISHI WA UMMA WAKUMBUSHWA KUTUNZA KUMBUKUMBU ZA KAZI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewakumbusha watumishi wa Ofisi yake kuweka na kutunza kumbukumbu za majukumu wanayoyafanya kila siku ili kusaidia vizazi vijavyo kufanya marejeo pale inapotakiwa kwa lengo la kuimarisha uendelevu wa taarifa katika utoaji wa huduma.
Bw. Daudi ameyasema hayo Aprili 20, 2026 wakati akihitimisha mafunzo ya uelewa kwa watumishi wa Ofisi yake kuhusu Mpango Endelevu wa Kushughulikia Majanga yaliyotolewa katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma.
Aliongeza kuwa, watumishi wa umma hawanabudi kuzingatia mafunzo ya kimkakati wanayopewa ili kuhakikisha yanawajengea uwezo stahiki wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
‘’Majukumu ya Serikali yanaishi, lakini watumishi wa Umma huondoka kutoka kituo kimoja kwenda kingine, hivyo nyaraka zote zinapaswa kuhifadhiwa ipasavyo kwa kuzingatia usalama na utaratibu unaofaa ili watumishi wanaobaki na watakaokuja waweze kurejerea’’ Bw. Daudi alisema.
Aidha Bw. Daudi amewataka viongozi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Ofisi yake kufuatilia na kujiridhisha iwapo mafunzo yanayotolewa kila jumatatu ya wiki yanaongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma na Mifumo ya TEHAMA Serikalini kutoka Ofisi ya Rais, UTUMISHI Bw. Tiba Manoni amesema, Taasisi yoyote ni lazima ihakikishe inaweka mipango endelevu ya kushughulikia majanga.
Kadhalika Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa majanga ya asili, ukosefu wa fedha, hitilafu za mifumo ya teknolojia na magonjwa ya mlipuko ni sehemu ya majanga yanayoweza kutokea na kupelekea kusitishwa kwa shughuli za utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma kwa umma.
