Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUSHUGHULIKIA HOJA ZILIZOPO KATIKA MFUMO WA e-MREJESHO


Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema mafunzo ya kutumia mfumo wa e-Mrejesho ni ajenda na kiashiria muhimu cha matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma kwa umma.

Bw. Daudi amebainisha kuwa utaratibu wa kushughulikia mrejesho wa Wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora ambayo inalenga kuzingatia na kujali matakwa na maslahi ya wengi, kuheshimu sheria, kuwa na uwazi, uwajibikaji, usikivu, haki na usawa, demokrasia, kupiga vita rushwa na kushirikisha umma katika utawala.

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa, watumishi wa umma hawana budi kusimamia ipasavyo eneo la usikivu na uwajibikaji kwa kuwapa wananchi fursa ya kuwasilikiliza ili Serikali kupitia Taasisi zake iweze kubaini maeneo yenye mapungufu na kubadili tabia na mienendo ya utendaji miongoni mwa Watumishi wa Umma.

“Ninawasihi kutekeleza kwa makini mliyojifunza kwa kuwa suala ya matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa umma katika Utumishi wa Umma ni utekelezaji wa maekelezo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona Serikali inatoa huduma bora kwa umma kwa haraka na kwa ufanisi” amesema Bw. Daudi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Maadili Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bi. Janet Mishinga amesema idara yake inaendelea kutoa mafunzo ya matumzi ya mfumo wa e-Mrejesho kwa taasisi za umma na  itafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mfumo huo kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto ili kuimarisha mfumo huo kwa lengo la kukuza Uadilifu katika Utumishi wa Umma.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya Usimamizi Maadili imehitimisha mafunzo ya siku nne (4) kwa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Afya na Maji kuhusu Mfumo wa Kielekroni wa Kutuma, Kupokea na Kufuatilia Malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi Serikalini (e-Mrejesho) yaliyoanza tarehe 28 Novemba hadi tarehe 1 Disemba, 2023 katika Ukumbi Mdogo wa Chuo cha VETA Jijini Dodoma.