Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUPIMA SARATANI


 

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Cyrus Kapinga, amewahimiza watumishi wa umma kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, hususan magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Saratani, ili kubaini changamoto za kiafya mapema na kupata matibabu yenye mafanikio.

 

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa semina ya elimu kuhusu saratani iliyofanyika katika Ofisi hiyo, amesema afya njema ya watumishi ni msingi wa kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Aidha, amesisitiza kuwa uchunguzi wa afya wa mara kwa mara unasaidia kugundua magonjwa katika hatua za awali, hivyo kurahisisha matibabu na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

 

Awali akitoa elimu kuhusu ugonjwa wa Saratani, Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani na Elimu Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam, Dkt. Maguha Stephano amesema Saratani ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuongezeka duniani na kusababisha vifo kila mwaka.

 

Amesema athari za Saratani zinaweza kuwa kubwa kwa mgonjwa, familia na jamii kwa ujumla, kwani ugonjwa huo unaweza kusababisha maumivu makali, ulemavu, kupunguza uwezo wa mtu kufanya kazi, kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na kuongeza gharama za matibabu.

“Ugonjwa huu hutokea pale seli za mwili zinapoanza kukua na kuongezeka bila mpangilio, hali inayoweza kushambulia viungo mbalimbali vya mwili kama vile matiti, mlango wa kizazi, tezi dume, mapafu, utumbo, ini na ngozi” amesema.

Akizungumzia baadhi ya sababu na vihatarishi vinavyosababisha uwezekano wa kupata saratani, Dkt. Maguha amesema matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji usiozingatia lishe bora, uzito uliopitiliza, kutofanya mazoezi ya mwili pamoja na kurithi vinasaba vinavyohusishwa na aina za saratani.

Sambamba na hayo,amesema Hospitali hiyo itaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kutoa elimu ya afya pamoja na huduma za uchunguzi wa saratani, ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuhamasisha kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Semina hiyo imetolewa kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni jitihada za kuendelea kuimarisha ustawi wa watumishi wa umma kwa kutoa elimu ya afya na kuhamasisha kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.