Habari
WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUONGEZA UWAJIBIKAJI KATIKA KUTOA HUDUMA BORA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewahimiza Watumishi wa Umma kuongeza uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi.
Bw. Daudi ametoa wito huo leo alipokuwa akiwapongeza Watumishi wa Ofisi hiyo waliozaliwa mwezi Machi, 2026 mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo yanayofanyika kila siku ya Jumatatu Mtumba Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuimarisha utendaji kazi watumishi wa ofisi hiyo.
Bw. Daudi amesema, mtumishi wa umma anapoongeza umri imsaidie kuongeza chachu ya utendajikazi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
''Nitoe wito kwa Watumishi wa Umma mnapoongeza umri na kusherehekea siku yenu ya kuzaliwa, hakikisheni mnawajibika ipasavyo katika maeneo yenu ya kazi hasa mnapotoa huduma kwa Watumishi wa Umma wenzenu na Wananchi, hakikisheni kuwa mnatimiza malengo ya Serikali katika kutoa huduma bora kwa kila Mtanzania.” amesema Bw. Daudi.
Awali katika mafunzo hayo, Afisa Rasilimaliwatu Mkuu kutoka katika ofisi hiyo, Idara ya Mishahara, Maslahi na Marupurupu, Bi. Magreth Banogile akiwasilisha mada kuhusu Motisha katika Utumishi wa Umma alisema, motisha ni manufaa anayoyapata mtumishi baada ya mshahara kutokana na majukumu anayoyatekeleza hivyo ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili aweze kupata stahiki ya motisha husika.
Ameongeza kuwa baadhi ya motisha katika Utumishi wa Umma ni pamoja na mazingira bora ya kazi, vitendea kazi, fursa za mafunzo, huduma ya usafiri wa kwenda na kurudi kutoka kazini, pamoja na fursa ya muda wa kufanya mazoezi.
Aidha, katika mafunzo hayo kulikuwa na mada mbalimbali zilizowasilishwa na Maafisa kutoka katika Idara hiyo ya Mishahara, Maslahi na Marupurupu ambapo Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi Bw. Baraka Kilagu aliwasilisha mada kuhusu Miundo ya Maendeleo ya Utumishi chini ya Wizara pamoja na Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi, Bw. Imani Mtumbi aliyewasilisha mada kuhusu Miundo ya Mishahara katika Utumishi wa Umma.
