Habari
WATUMISHI WA UMMA WAHIMIZWA KUJIENDELEZA KATIKA TAASISI WANAZOFANYA KAZI
Watumishi wa umma wamehimizwa kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma katika Taasisi wanazofanya kazi ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma wanazozitoa kwa umma.
Wito huo umetolewa na Mwezeshaji, Bw. Moses Raymond, alipokuwa akiwasilisha mada kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu “Ukuaji Binafsi na Kitaaluma kwa Utendaji Endelevu wa Taasisi” (Personal and Professional Growth for Sustainable Organisational Performance).
Bw. Raymond amesema umuhimu wa kuongeza maarifa na ujuzi katika utekelezaji wa majukumu yao unasaidia kwenda sambamba na ukuaji wa teknolojia, mabadiliko ya Sera na mahitaji ya wananchi. Hivyo, ametoa rai kwa watumishi wa umma kuwa tayari kujifunza.
“Mtumishi anayejifunza mara kwa mara huwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto, kutumia teknolojia kwa ufanisi na kutoa huduma zinazokidhi viwango vinavyohitajika. Aidha, kujiendeleza kunawasaidia watumishi kuelewa vizuri sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma”.
