Habari
WATUMISHI WA UMMA KUJITATHMINI KUPITIA KONGAMANO LA SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb) amesema maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kwa mwaka 2024 yamekuja na fursa ya Kongamano mahususi kwa ajili ya Watumishi wa Umma kujitathmini ni kwa namna gani wanawajibika kwa Umma na kutekeleza jukumu la Serikali la Ustawi wa Wananchi kwa kuzingatia Haki za Binadamu na kuepuka vitendo vya rushwa.
Mhe. Simbachawene amesema hayo Disemba 5, 2024 katika Ukumbi wa NAOT Dodoma wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika uzinduzi wa siku ya maadili na haki za binadamu.
“Ninaamini, Watumishi wa Umma watatumia fursa ya uwepo wa Kongamano hilo kujitathmini kuhusu uzingatiaji wa Haki za Binadamu na kuepuka rushwa wanapotoa huduma kwa Umma”. alisema Mhe. Simbachawene.
Aidha, katika Kongamano hilo, zitawasilishwa na kujadiliwa mada mbili ambazo ni Haki za Binadamu katika Mapambano Dhidi ya Rushwa” na “Maadili, Haki na Wajibu wa Watumishi wa Umma. Mada hizo zimezingatia Kaulimbiu ya mwaka 2024 isemayo “Tumia haki yako ya Kidemokrasia, chagua viongozi waadilifu na wanaozingatia Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora kwa maendeleo ya Taifa letu”
Sambamba na Kongamano hilo, Taasisi Simamizi za Utawala Bora zitafanya ziara kwenye Magereza ya Kongwa na Mpwapwa Mkoani Dodoma na kuwasikiliza wafungwa na mahabusu na kutoa misaada ya kijamii.
Kila tarehe 10 Desemba, Tanzania huungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Kimataifa ikiwa ni utekelezaji wa Tamko la Haki za Binadamu liililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 10 Desemba, 1948 (Universal Declaration of Human Rights - UDHR).
Taasisi zinazoshirikiana katika kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa ni pamoja na Ofisi ya Rais, Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani.