Habari
WATUMISHI WA UMMA KUJAZA KAZI WANAZOFANYA KATIKA MFUMO MAHALI POPOTE
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais- UTUMISHI ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa kuhimiza uwajibikaji wa hiari wa mtumishi kwa kujaza kazi anazofanya kila siku katika mfumo mahali popote ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa umma.
Ameyasema hayo leo tarehe 12 Desemba, 2023 wakati wa kufungua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini (HR Assesment) kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Bi. Felista amefafanua kuwa mfumo wa PEPMIS utawezesha viongozi kusimamia utendaji kazi wa watumishi bila upendeleo na utaongeza ufanisi, PIPMIS itawezesha kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma na HR Assesment itawezesha kufanya Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini na kuitumia ipasavyo.
Aidha, Bi. Shuli ameongeza kuwa hali ya mafunzo kwa Mkoa wa Dodoma inaendelea vizuri na anaamini yatakamilika kama ilivyopangwa kwa kuwa pande zote zinazohusika na mafunzo zinatoa ushirikiano mkubwa kwa wakati.
“Wawezeshaji wote wako vizuri na watumishi kutoka katika Wizara na Taasisi zote wanaitikia wito na wanakuja na kompyuta ambazo ni kitendea kazi muhimu sana katika mafunzo haya” amesema Bi.Felista.
Vilevile, amesema mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa OPRAS ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayowezesha viongozi na watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakati na mahali popote.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha Bw. Renatus Msagira amesema watumishi wako tayari kujifunza na kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi kwa maendeleo ya taifa.
“Tuko tayari na hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa jitihada hizi muhimu za Serikali ambazo lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati” amesisitiza Bw. Msagira.
Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment yanaendeshwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mikoa yote Tanzania Bara na yatahitimishwa Desemba 31,2023.