Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA UMMA KILOSA, MIKUMI NA DUMILA WAPATA MAFUNZO YA MATUMIZI YA MIFUMO YA TEHAMA


Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro, Bw. Priscus Kiwango amewataka watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wao na taasisi kwa jumla.

Bw. Kiwango amesema mifumo hii itawawezesha viongozi kusimamia utendaji kazi wa watumishi wao bila upendeleo ikiwemo kupanda vyeo kwa haki, kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma na kufanya Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma.

Amesema hayo katika nyakati tofauti wakati wa mafunzo ya namna ya kutumia mifumo mipya ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Watumishi wa Umma na taasisi zilizopo mkoani Morogoro katika Kanda tatu ikiwemo Mikumi, Kilosa Mjini na Dumila.

Mkurugenzi Kiwango ameongeza kuwa mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwenye Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Gairo, Morogoro mjini na kwa baadhi ya taasisi na kwa watendaji wa kata na vijiji, walimu wa sekondari na msingi, watumishi wa kilimo, mifugo na ustawi wa jamii.

“Mpaka sasa kwa mkoa wa Morogoro tumetoa mafunzo kwa taasisi 21 ikiwemo Ofisi ya RAS, Halmashauri ya Morogoro DC, Manispaa ya Morogoro, Mvomero, Malinyi, Mlimba, Ifakara Ulanga, Kilosa, Mikumi na Dumila na kwa mwenendo huu tutakamilisha mafunzo kwa wakati uliopangwa”. Alisema Bw. Kiwango.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia huduma za Uuguzi na Ukunga nchini, Wizara ya Afya, Bw. Paul Mashauri amesema watumishi wa umma mkoa wa Morogoro wanaonesha utayari wa kutumia mifumo hii katika utendaji kazi wao kutokana na uwazi uliopo katika mifumo.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Matilda Mtenga ambaye pia ni mkufunzi ameongeza kuwa, mwitikio wa watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro ni mkubwa na wanafurahi kuona ujio wa mifumo inayonesha uwezo wa  kila mtumishi wa umma.

Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kutoa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment katika Mikoa yote Tanzania Bara na yanatarajiwa kuhitimishwa Desemba 31,2023.