Habari
WATUMISHI WA UMMA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA WAISHUKURU SERIKALI KUANZISHA MRADI WA UJENZI WA MAKAZI NCHINI
Watumishi wa Umma wa Kituo cha Afya Kilagano na Shule ya Sekondari Jenista Mhagama waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea wameishukuru Serikali kupitia Timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na Watumishi Housing Investments kwa kuanzisha Mradi wa Ujenzi wa Makazi kwa Watumishi wa Umma nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi hao, Mkuu wa Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, Bi. Felister Kulwambalo amesema, Watumishi wa Shule ya Sekondari Jenista Mhagama wanaishukuru Serikali kupitia timu hiyo kwa kusimamia, kukagua na kufanya tathmini ya mwisho ya kukamilika kwa mradi huo na kuahidi watakapokabidhiwa tija ya utendaji kazi itaongezeka.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuona umuhimu wa kutujengea makazi bora, tunaahidi tutakapokabidhiwa rasmi nyumba hizi tija ya utendaji kazi itaongezeka sana, lakini pia adha ya watumishi kutoka umbali mrefu kuja katika eneo la kazi itapungua,” amesema Bi. Kulwambalo
Timu hiyo ya Wataalam imeongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Patrick Allute wakati wa ziara ya kikazi waliyoifanya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma kwa lengo la kukagua na kufanya tathmini ya mwisho ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma utakaosaidia kuondokana na changamoto ya makazi kwa watumishi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mradi huo wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma kwa awamu ya kwanza umetekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Lindi, Pwani na Ruvuma.
