Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA OFISI YA RAIS-UTUMISHI WASISITIZWA KUZINGATIA ITIFAKI NA DIPLOMASIA KATIKA UTENDAJI KAZI


Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wamesisitizwa kuzingatia Itifaki na Diplomasia katika utendaji kazi Ili kujenga heshima ya ofisi kwa manufaa ya nchi.

Wito huo umetolewa leo Januari 27, 2025 na Balozi Nelson Lyimo (mstaafu) wakati akifanya wasilisho kuhusu Itifaki na Diplomasia kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Balozi Lyimo amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ni muhimu kwa Taifa la Tanzania kwa kuwa inasimamia rasilimaliwatu, hivyo Watumishi wake wanatakiwa kuzingatia Itifaki na Diplomasia wakati wote wanapotekeleza majukumu yao katika ofisi hiyo.

Amewasisitiza Watumishi kuwa wasikivu kwa wateja wanaowahudumia na kuona namna ya kuwasaidia kupata majibu au suluhisho la suala ambalo mteja husika ameliwasilisha.

“Niwaombe kila mtumishi wa ofisi hii ajipime namna anavyotoa huduma kwa wateja kwani ndio kipimo cha tabia njema wakati wa utendaji kazi, jambo ambalo litaenda kuitangaza ofisi vizuri kwa maslahi mapana ya taifa,” amesisitiza Balozi Lyimo.

Akihitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Bw. Musa Magufuli alimshukuru Balozi Lyimo kwa kutoa elimu hiyo kwa watumishi hao ambayo itaboresha utendaji kazi kwa watumishi wao.

Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliandaa utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wake kila Jumatatu ya wiki kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ustawi wa Taifa.