Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI WA OFISI YA RAIS, UTUMISHI WANOLEWA KUHUSU MFUMO WA e-UTENDAJI


 

 

 

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.  Priscus Tairo ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuchukua muda wao kujifunza kwa undani Mfumo  wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma ili kuwa msaada kwa watumishi walio nje ya Ofisi hiyo ambao wamekuwa wakihitaji kupata mafunzo ya mfumo huo ili waweze kuutekeleza kwa ufanisi.  

 

Bw. Tairo ametoa kauli hiyo  leo Jumatatu Disemba 02, 2024 Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma wakati akitoa  mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Ofisi hiyo,  ikiwa ni muendelezo wa kutoa mafunzo elekezi ya kila wiki kwa Watumishi  hao  kwa  lengo la  kuboresha utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma nchini.

 

Bw. Tairo amesema Mfumo huu ni mpya, hivyo unahitaji watumishi wengi wenye uwezo wa kutoa msaada wa kiufundi kwa ukaribu, haraka na ufanisi ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

 

Amesema endapo Watumishi wa Ofisi hiyo wataweza kuufahamu vizuri jinsi mfumo huo wa e- unavyotenda kazi utawawezesha kutoa msaada kwa watumishi wengine wakati wowote na mahali popote lengo likiwa ni  kuifanya Serikali iweze kubaini mwenendo halisi wa utendaji kazi wa watumishi wa umma nchini.

 

Kufuatia hatua hiyo, Bw. Tairo  amewataka Watumishi wa Ofisi hiyo kutumia muda wao  mwingi kujinoa katika eneo hilo kwani Watumishi wa nje ya Ofisi hiyo wana imani kubwa na watumishi wa Ofisi hii  bila kujali wanatoka katika idara inayojihusisha na mafunzo hayo.