Habari
WATUMISHI WA OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA WAASWA KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO WAO

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wametakiwa kuwa karibu na watoto wao huku wakiaswa kufuatulia mienendo ya watoto hao ili kuwa na jamii bora
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatatu, Julai 21, 2025 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. Christer Kayombo,ikiwa ni muendelezo wa mafunzo ambayo hutolewa kila jumatatu ya wiki kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora
Amesema visa vingi vya ukatili vinavyotokea katika jamii hususani kwa watoto vimekuwa vikichangiwa na baadhi ya wazazi na walezi ambao hawawajibiki ipasavyo katika suala zima la malezi ya watoto wao.
Amewataka Watumishi hao kuwa kioo kwenye jamii kwa kuwalea watoto wao kwenye maadili mema huku akiwataka watumishi hao kuzingatia maadili mema pamoja na kuimarisha mahusiano katika familia zao.
"Tengeni muda wa kufuatulia mienendo ya watoto pindi mnapotoka katika majukumu yenu, msitoe mianya ya uhalifu pamoja na vitendo vya ukatili kufanyika majumbani kwa kuwaachia wafanyakazi wa majumbani kuwalea watoto wenu, hakikisheni mnasimama kwenye nafasi zenu kama walezi" amesisitiza ASP. Kayombo.
Katika hatua nyingine, ASP. Kayombo amewataka Watumishi hao kuwa mabalozi wazuri wa kupinga ukatili majumbani,maofisini pamoja na jamii inayowazunguka.
" Ni matumaini yangu baada ya mafunzo haya vitendo vya ukatili kwa watoto na matendo yasiyofaa katika jamii yatakwenda kupungua" amesema ASP. Kayombo