Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WASISITIZWA KUZINGATIA UANDISHI WA NYARAKA ZA SERIKALI


Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wamesisitizwa kuzingatia uandishi wa Nyaraka za Serikali ikiwemo barua, dokezo na taarifa mbalimbali ili kurahisisha mawasiliano ndani ya ofisi baina ya Idara na Vitengo.

Mchambuzi kazi, Idara ya Usimamizi wa Taasisi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Macdonald Kiwia ameyasema hayo leo tarehe 16 Desemba, 2024 wakati akiwasilisha mada kuhusu Mwongozo wa Uandishi wa Nyaraka mbalimbali za Serikali wakati wa mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo Viongozi na Watumishi wa ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Aidha, Bw. Kiwia ametoa wito kwa watumishi hao kuzingatia Sheria, Kanuni Taratibu na Miongozo mbalimbali ya uandishi wa Nyaraka za Serikali ili kuboresha utendajikazi kwa watumishi hao na watumishi wa umma nchini kote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli amewasisitiza watumishi wa ofisi hiyo kuhudhuria mafunzo hayo bila kukosa kila siku ya Jumatatu kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi wote na kuwa na uelewa wa pamoja wa matumizi sahihi ya masuala mbalimbali kuhusu Utumishi wa Umma.