Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAASWA KUBADILI MFUMO WA MAISHA ILI KUJIEPUSHA NA MARADHI YASIYOAMBUKIZA


Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wametakiwa kuzingatia na kubadili mfumo wa maisha ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza kwa lengo la kuwahudumia wananchi pasipokuwa na changamoto zozote za kiafya.

Wito huo umetolewa leo February 24, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge wakati akiwasilisha mada kuhusu afya kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Dkt. Kisenge amesema Magonjwa ya Kisukari na Shinikizo la damu yanatokana na namna watu wanavyoendesha maisha yao hivyo, ni vema kupunguza matumizi makubwa ya sukari na matumizi ya ulaji wa chumvi nyingi inayosababisha shinikizo la juu la damu ambalo moja ya madhara yake ni kutanuka kwa moyo ambao matibabu yake ni gharama kubwa.

Aidha, Dkt. Kisenge amewataka watumishi wa ofisi hiyo kujitahidi kutumia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora ili kukabiliana na magonjwa ya moyo.

Dkt. Kisenge ametoa wito kwa watumishi hao kupima afya zao mara kwa mara ili kujua tatizo mapema pamoja na kupunguza gharama za matibabu kwani ugonjwa ukishakuwa mkubwa gharama huongezeka zaidi.

Akihitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amemshukuru Dkt. Kisenge pamoja na wataalamu alioambatana nao kwa kutoa elimu hiyo kwa watumishi wa ofisi yake na kuahidi kuzingatia suala la afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ustawi wa Taifa la Tanzania.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Rais –UTUMISHI wa kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.