Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WARATIBU WA TASAF HANDENI WAPONGEZWA KWA KUWASHIRIKISHA VIONGOZI WAO KATIKA MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI YA TASAF


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewapongeza Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kwa kuwashirikisha viongozi wao kuhusu matumizi ya fedha za miradi ya TASAF inayopelekwa katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa maendeleo ya miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

“Ninawapongeza Waratibu wa TASAF katika Halmashauri hii ya Handeni kwa kuwashirikisha viongozi wenu katika matumizi ya fedha zinazoletwa na TASAF, ushirikiano huu ni mzuri kwa sababu fedha hizi zinatakiwa zitumike kwa uwazi ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Amesema viongozi wengi katika Halmashauri za Wilaya hawana taarifa juu ya fedha za miradi ya TASAF zinazoingia katika Wilaya zao lakini imekuwa tofauti kwa Wilaya ya Handeni, ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo katika maelezo yake anaonekana kuufahamu vizuri utekelezaji wa mradi huu.

“Mkuu wa Wilaya, nimefurahi sana kuona kuwa mradi huu unauelewa vizuri maana umeuzungumzia vizuri sana, hii inaonyesha kuwa unashirikishwa kikamilifu, na hivi ndivyo inavyotakiwa,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Amemsisitiza Mkuu wa Wilaya hiyo ya Handeni Mhe. Albert Msando kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kuwaachia waratibu pekee kwa kuwa fedha za miradi zinazopelekwa ni nyingi, hivyo zinahitaji usimamizi ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Simbachawene amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu ya kuzungumza na watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri za Wilaya ya Mkinga, Korogwe na Handeni mkoani Tanga.