Habari
WARATIBU WA KUDHIBITI VVU, UKIMWI NA MAGONJWA SUGU YASIYOAMBUKIZA WATAKIWA KUTOA ELIMU JUU YA UDHIBITI MAGONJWA MAHALI PA KAZI ILI KUFIKIA MALENGO YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Waratibu wa ngazi ya Mikoa Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutoa elimu kwa watumishi wa umma juu ya udhibiti wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga taifa lenye watu wenye afya, tija, ustawi na ufanisi ambao watatoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uchambuzi Sera wa ofisi hiyo, Dkt. Charles Kato wakati akifungua semina elekezi kwa Waratibu wa ngazi ya Mikoa kuhusu udhibiti wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza Mahali Pa Kazi katika Utumishi wa Umma iliyofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Kato amesema katika kutekeleza afua za kuimarisha afya kwa watumishi ni vema kuwa na program za upimaji wa afya pamoja na mazoezi ya viungo kwa watumishi katika maeneo yao ya kazi ili kufikia utekelezaji huo wa Dira 2050.
Ameongeza kuwa, itakuwa vema kuandaa mafunzo pia kwa watumishi pamoja na msaada wa kisaikolojia ili kuwasaidia zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Dkt. Kato amewataka waratibu hao kuandaa taarifa za utekelezaji wa Mwongozo na Waraka Na. 2 wa mwaka 2014 kuhusu kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukiza Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Menejimenti Anuai za Jamii ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu, Bi. Herieth Mpili akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kukuza uelewa na ufahamu juu ya majukumu ya Waratibu hao na kuwawezesha kuandaa mipango ya muda mrefu na mfupi wa utekelezaji wa afua za kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa yote nchini kwa lengo la kusimamia masuala ya Anuai za Jamii na kutoa mafunzo kwa maafisa au waratibu watakaoteuliwa kuratibu afua hizo katika mikoa yao ili kuhakikisha kunakuwa na afya imara na ustawi wa watumishi wote nchini.
