Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WANAMICHEZO UTUMISHI WAPEWA HAMASA KUELEKEKEA MASHINDANO YA MEI MOSI SINGIDA


“Ninaamini wote tuna afya njema na tuko tayari kupambana na kuendelea kulinda taswira njema ya ofisi yetu, kwa hiyo twendeni tukashiriki mashindano hayo tukiwa na umoja na ari kubwa, tukilenga kurudi na vikombe vingi zaidi ya mwaka 2024”

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi wakati wa kikao kifupi kilichofanyika katika jengo la ofisi za Utumishi, Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kuwaaga Viongozi na Wanamichezo wa ofisi yake wanaokwenda Mkoani Singida kushiriki Mashindano ya Michezo ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Bw. Daudi aliwasisitiza viongozi na wanamchezo hao kushiriki michezo yote kikamilifu na kuzingatia sheria na kanuni za michezo zilizoandaliwa ili kupata ubingwa na vikombe vingi zaidi kuliko kipindi kilichopita.

Aidha, aliwataka watumishi hao kuwa na nidhamu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa wamebeba sura chanya ya ofisi ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia maadili ndani ya Utumishi wa Umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendelezaji Taasisi na Mlezi wa Wanamichezo hao Bw. Nolasco Kipanda alisema kuwa mwaka 2024 wakati wa mashindano ya SHIMIWI Ofisi ilishinda Makombe Matatu (3) ikiwa ni pamoja na kombe la mpira wa miguu, hivyo amewahimiza wanamichezo hao kuongeza jitihada zaidi ili kuleta heshima kubwa hata katika mashindano ya Mei Mosi.

Bw. Kipanda kwa niaba ya Wanamichezo hao amewashukuru na kuwapongeza Viongozi na Timu ya Menejimenti kwa upendo na ushirikiano wanaoonesha katika michezo hadi kupata mafaniko ya kushinda makombe katika mashindano mbalimbali.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili Bi. Leila Mavika amewataka wanamichezo hao kuwa na maadili mema wakati wote na kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi na kukosa staha.

“Nawakumbusha kutunza mbinu na taarifa nyingine za kambi na kuheshimu sheria, kanuni na miongozo inayoongoza Utumishi wa Umma na michezo ambayo tunaenda kishiriki” alisisitiza Bi. Mavika

Awali, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw. Musa Magufuli amesema jumla ya Watumishi 57 wameruhisiwa kwenda Mkoani Singida kwa ajili ya kushiriki mashindano ya siku ya Wafanyakazi Duniani na Ofisi itashiriki michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa pete, karata, riadha na bao ambayo inatarajiwa kuanza Aprili 15, 2025.