Habari
WAKUU WA IDARA ZA UTAWALA NA USIMAMIZI WA RASILIMALIWATU KATIKA SEKTA ZA UMMA KUSHIRIKI KIKAO KAZI
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi ametoa wito kwa Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kuhudhuria na kushiriki Kikao Kazi ili kubadilishana uzoefu na kupata maelekezo kuhusu masuala yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika utumishi umma kwa kuzingatia Shabaha na vipaumbele vya Taifa.
Bw. Daudi ametoa wito huo leo wakati alipokuwa akizungumza na Wandishi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi hizo Mtumba, Jijini Dodoma kuhusu Kikao Kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara zinazojitegemea, Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kitakachofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
“Ninatoa wito kwa Maafisa Masuhuli wote kuwaruhusu Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimawatu Serikalini kujisajili kwenye mfumo https://tsms.gov.go.tz na mwisho wa kujisajili ni tarehe 13 Desemba, 2024” alisema Bw. Daudi.
Aidha, alibainisha kuwa na washiriki wote watatakiwa kufika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo katika Mji wa Serikali Mtumba tarehe 16 Disemba, 2024 kuanzia saa 10:00 jioni ili kuchukua vitambulisho na makabrasha ya kikao.
Kikao hicho kitaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala ya Kidijitali iliyoboreshwa” na Mgeni Rasmi wa Ufunguzi atakuwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu mbalimbali kwa mujibu wa Hati ya Mgawanyo wa Majukumu kwa Mawaziri kama ilivyotangazwa katika Gazeti la Serikali Toleo Na. 619A & 619B la tarehe 30/8/2023. Moja ya majukumu hayo ni kusimamia Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma na Utawala wa Utumishi wa Umma.