Habari
WADAU WASISITIZWA KUJADILI MIFUMO SAHIHI YA URATIBU WA AJIRA ZA RAIA WA KIGENI KWA MANUFAA YA WATANZANIA

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cyrus Kapinga, amesema Serikali inatambua mchango wa wataalamu wa kigeni katika nyanja mbalimbali za maendeleo, lakini ni muhimu kuweka mifumo sahihi ya uratibu ili kuhakikisha ajira hizo zinakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.
Bwana Kapinga ameyasema hayo leo tarehe 2.9.2025 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Wadau wa Ajira za Raia wa Kigeni kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Idara zinazojitegemea chenye lengo la kujadili Rasimu ya Mwongozo wa Kuratibu Ajira za Raia wa Kigeni katika Utumishi wa Umma.
“Kikao hiki kimewaleta pamoja ili muweze kutumia uzoefu na utaalam mlionao kujadili ipasavyo, kupata maoni yatakayoboresha rasimu hiyo na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo bila kusahau uzingatiwaji wa Tamaduni, Desturi na Maadili ya Kitanzania, ninawahimiza kushiriki kikamilifu ili kikao kiwe na tija iliyotarajiwa.” Bw. Kapinga amesisitiza.
Bw. Kapinga amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mujibu wa Hati idhini imepewa jukumu la kusimamia Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ikiwemo kuratibu ajira za wataalam raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi katika Sekta mbalimbali za Umma nchini wanaopatiwa vibali vya kufanya kazi na ukaazi vyenye msamaha wa ada.
Ameongeza kuwa, Ajira za wataalam raia wa kigeni zimekuwa zikiratibiwa kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi Na. 1 wa mwaka 2000 kuhusu Ajira za Raia wa Kigeni katika Utumishi wa Umma. Pamoja na Waraka huo, Sheria ya Ajira za Raia wa Kigeni Sura 436 ziliandaliwa mwaka 2015 na Kanuni zake za Mwaka 2016 ili kuimarisha uratibu wa ajira hizo na kuendana na mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza. Hata hivyo pamoja na kuanzishwa kwa Sheria hiyo, Waraka Na. 1 wa mwaka 2000 umeendelea kutumika katika kuratibu ajira za raia wa kigeni.
Amesema katika kuratibu ajira hizo, Ofisi imekuwa ikikutana na changamoto za Waajiri kutozingatia matakwa mbalimbali ikiwa ni vigezo muhimu vilivyoainishwa katika nyaraka zinazosimamia Ajira kwa Raia wa Kigeni.
Ameainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni maombi ya vibali vya kazi kuwasilishwa wakati wataalam raia wa kigeni wakiwa wameingia nchini, baadhi ya Kamati za Ushauri wa Ajira za Raia wa Kigeni kutokukaa vikao kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi Na.1 wa mwaka 2000 kuhusu Ajira za Raia wa Kigeni hivyo maombi kuwasilishwa yakiwa hayana mihutasari yenye uhalisia, Kamati kutokuchambua ipasavyo maombi yanayowasilishwa. “Haya yote niliyoyataja ni kinyume cha utendaji kazi kwa mujibu wa miongozo tuliyonayo.” Bw. Kapinga ameongeza.
Amesema changamoto hizo zote zimekuwa zikisababisha ucheleweshwaji wa uratibu wa maombi ya vibali na kusababisha malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa Waajiri wa wataalam hao.
“Ili kukabiliana na changamoto hizo, Ofisi imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa Kuratibu Ajira za Raia wa Kigeni katika Utumishi wa Umma utakaotoa maelekezo mahsusi ya namna bora ya kuratibu ajira hizo.” Amesisitiza Bw. Kapinga.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao kazi hicho walipongeza hatua hiyo na kuahidi kushirikiana kikamilifu katika kutoa maoni yatakayosaidia kukamilisha mwongozo huo. Wadau walisisitiza umuhimu wa kuweka vigezo vinavyohakikisha ajira za kigeni zinakuwa za kiufundi na kitaalamu pale ambapo ujuzi huo haupo nchini.