Habari
VIONGOZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA WASISITIZWA KUTUMIA FURSA YA MAFUNZO WANAYOYAPATA KUIMARISHA UTENDAJIKAZI KWA USTAWI WA TAIFA

Viongozi katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutumia kikamilifu fursa ya mafunzo wanayoyapata kutoka Serikalini na kwa wadau mbalimbali ili kuimarisha utendaji kazi kwa ustawi wa taifa.
Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, SACP. Ibrahim Mahumi wakati akifunga mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Sekretarieti za Mikoa, Wizara na Taasisi za Umma yaliyolenga kuwajenga kifikra, kitabia na mtazamo kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa mafunzo kwa viongozi kutokana na dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samila Suluhu Hassan ya kuhakikisha viongozi kwenye Utumishi wa Umma wanakuwa na uelewa mpana utakaowasaidia kutekeleza majukumu ya serikali kikamilifu.
SACP. Mahumi amesema, mafunzo hayo yamejumuisha kundi la kuanzia mwezi Agosti 2021 hadi 2024 lenye viongozi 62 kutoka Wizara 11, Taasisi za Umma 8 na Sekretarieti za Mikoa 16.
Ameongeza kuwa, makundi mengine ya viongozi ambayo hayajafikiwa katika mafunzo hayo, watapatiwa kulingana na mipango iliyowekwa na serikali katika kuhakikisha kila kiongozi kwenye utumishi wa umma anapata mafunzo elekezi kwa lengo la kuboresha utendajikazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amesema Idara anayoiongoza imekuwa ikitoa mafunzo kwa Viongozi na watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Bi. Mavika amesema viongozi hao wamepata nafasi ya kujifunza masuala ya maadili, kupata uzoefu kutoka kwa baadhi ya viongozi wastaafu, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, itifaki na ustaarabu pamoja na utamaduni wa kitaasisi.
Aidha, Mkurugenzi Mavika amesema mafunzo ni suala endelevu, hivyo viongozi na watumishi wanapaswa kuendelezwa kwa kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ya kazi ili wafahamu namna ya kutekeleza majukumu yao.
Naye, Mkurugenzi Idara za Tawala za Mikoa-TAMISEMI, Bi. Beatrice Kimoleta ameipongeza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuandaa mafunzo hayo kwa viongozi wa Mikoa na Halmashauri ambayo yatawasaidia kushughulikia masuala mbali mbali yanayowahusu watumishi wa umma na wananchi.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu imehitimisha mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Sekretarieti za Mikoa, Wizara na Taasisi za Umma yaliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Jiji Dodoma.