Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

UZINGATIAJI WA ITIFAKI KATIKA UTUMISHI WA UMMA KUONGEZA UWAJIBIKAJI NA UADILIFU KIUTENDAJI


Katibu Mkuu ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ametoa rai kwa Watumishi wa Umma kuzingatia Itifaki katika Utumishi wa Umma ili kuongeza uwajibikaji na uadilifu kiutendaji kwa maslahi mapana ya Taifa.

Bw. Mkomi ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo katika eneo maalum la mafunzo kwa watumishi hao mara baada ya mkufunzi aliyekuwa akitoa mafunzo kuhusu Itifaki kuhitimisha mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa  kwa lengo la kuwajengea uwezo na uelewa wa Itifaki katika Utumishi wa Umma.

Akiwasilisha mada kuhusu Itifaki, Mwezeshaji wa Mafunzo, Mhadhiri wa Diplomasia, kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Bw. Lucas Humo amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora ina majukumu mengi ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali za kiutumishi hivyo, ni muhimu kila mtumishi akajua wajibu wake ili aweze kuwahudumia Viongozi, Watumishi wa Umma na Wananchi kwa kuzingatia Itifaki mbalimbali zitakazosaidia kuonesha taswira nzuri ya ofisi.

Aidha, Bw. Humo amesema, Itifaki inahusisha namna inavyopaswa kuwasiliana, kushirikiana, na kufanya maamuzi kwa njia inayoheshimu sheria na taratibu zilizowekwa.

“Watumishi wa umma wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu na uwazi kwa namna ya kuwasiliana, kushirikiana na kufanya maamuzi hivyo, wakifuata Itifaki na kuzitekeleza kwa ufanisi itaboresha utendaji kazi”, amesema Bw. Humo.

Bw. Humo, amewaasa watumishi hao kutunza taarifa za ofisi, kuzingatia muda wa kazi wakati wa kuingia na kutoka, kuwajali wageni wanapowasilisha masuala yao ya kiutumishi, kuzingatia mavazi wanapokuwa katika eneo la kazi pamoja na kuwatambua wageni wanapofika katika ofisi hiyo kwa vyeo vyao ili kutoa huduma kwa haki na usawa.