Habari
UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI WA MAKAZI KWA WATUMISHI WA UMMA KUONGEZA CHACHU YA UTENDAJIKAZI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na Watumishi Housing Investments (WHI) imehitimisha ziara ya kikazi katika Mikoa ya Singida, Ruvuma, Lindi, Pwani na Dodoma iliyolenga kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa makazi kwa Watumishi wa Umma.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Patrick Allute, amesema watumishi wa umma wanafurahia utekelezaji wa mradi huo ambao wanaamini utaleta motisha ya utendajikazi kwa kuwa karibu na eneo la kazi lenye makazi bora.
Kwa niaba ya timu hiyo Mkurugenzi Allute ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuwathamini watumishi wa umma kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi.
Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya fedha, Bw. Ezekiel Odipo ameeleza kuwa, Serikali inawajali watumishi wa umma hivyo imetoa fedha za kutosha ili kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo utekelezaji wa mradi wa makazi ya watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa jamii.
Naye, Mhandisi Salum Chanzi kutoka Watumishi Housing Investments, amesema WHI ndiyo kandarasi inayojenga makazi katika mradi huo ambao kwa sasa umefikia 85%.
Aidha, Mhandisi Chanzi amesema makazi hayo yatakuwa na ubora wa hali ya juu utakaoongeza ufanisi wa kazi kutokana na mazingira bora watakayokuwa nayo watumishi wa umma.