Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

UTAWALA BORA NA USIMAMIZI MAKINI WA RASILIMALIWATU NI MSINGI WA UTUMISHI WA UMMA WENYE MATOKEO – MHE. QWARAY


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria katika Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Qwaray ameyasema hayo Juni 3, 2026 wakati akifunga Kikao Kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi waRasilimaliwatu Serikalini kilichowakutanisha viongozi kutoka Wizara, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa Jijini Dodoma.

Amesema, mafanikio ya Serikali yanategemea kwa kiwango kikubwa ubora wa usimamizi wa rasilimaliwatu.

“Rasilimaliwatu ndiyo injini ya maendeleo ya taifa; isimamiwe kwa weledi, haki na uwajibikaji.” – Mhe. Regina Qwaray alisema.

Aidha Mhe. Qwaray alibainisha kuwa Serikali imeendelea kupokea malalamiko yanayohusiana na ucheleweshaji wa kupandishwa vyeo, malipo ya stahili za watumishi na ukiukwaji wa taratibu za kiutumishi, hivyo kuwataka wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu kuwa washauri waaminifu kwa viongozi wao na walinzi wa utawala wa sheria katika taasisi wanazozihudumia.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, matumizi salama ya teknolojia na ulinzi wa taarifa za Serikali, huku akitoa wito kwa waajiri kuwajengea watumishi uwezo kuhusu matumizi sahihi ya Akili Unde (AI) na mifumo ya kidijiti.

Katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, aliagiza utekelezaji wa Mfumo wa e-Utendaji usimamiwe kwa ukaribu zaidi, na kwamba wasimamizi watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kutathmini utendaji wa watumishi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa kufungwa kwa kikao hicho hakumaanishi mwisho wa juhudi za kuboresha Utumishi wa Umma, bali ni hatua ya kuanza kutekeleza kwa vitendo maazimio na maelekezo yaliyokubaliwa.

Kumalizika kwa kikao hiki si mwisho wa kazi, bali ni mwanzo wa utekelezaji wa maazimio na maelekezo yaliyotolewa kwa lengo la kujenga Utumishi wa Umma sikivu, jumuishi, na wenye matokeo,” alisisitiza Mhe. Qwaray.

Kwa upande wake Katibu Mkuu-UTUMISHI Bw. Juma Mkomi amesema ni matarajio yake kuwa kikao hicho kitaleta matokeo chanya kwa viongozi hao yatakayoboresha utekelezaji wa majukumu na kuongea tija katika utumishi wa umma.